01 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Majambazi Dar yakomba milioni 60
 
2009-05-01 16:30:47
Na Mwanaidi Swedi, Jijini

Wakati leo ikiwa ni siku ya Sikukuu ya Wafanyakazi duniani kote almaarufu kama Mei Mosi, majambazi Jijini wamepeleka kilio kwa baadhi yao baada ya kukomba jumla ya shilingi milioni 60 zinazodaiwa kuwa ni za mishahara.

Tukio hilo limetokea jijini jana pale katika maeneo ya Mtoni Bank Club, barabara ya Mandela ambapo majambazi hao watatu, wakiwa na bastola, waliwateka na kisha kuwapora mishara wafanyakazi wa kampuni ya Media Express Corporate.

Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Rukia Simbakalila amesema kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa 5:30.

Kamanda amesema majambazi watatu, wawili kati yao walivalia sare za Jeshi walisimamisha gari aina ya Corsa lenye namba za usajili T 803 AMC lililokuwa na dereva pamoja na Afisa Masoko wa Kampuni ya Media Express Cooperate.

Akasema baada ya kulisimamisha walimweleza dereva Seleman Waziri Mohamed, 29, kuwa gari hilo lilikuwa likitafutwa na Polisi baada ya kusababisha ajali na kuwa taarifa zake ziko Kituo cha Polisi Chang`ombe.

Kamanda Simbakalia akasema baada ya kumweleza Dereva kosa hilo wakafungua mlango wa gari na kuingia ndani huku wakimpa maelekezo ya kuelekeza gari katika Kituo cha Polisi Chang\'ombe.

Akasema walipofika maeneo ya Bandarini katika barabara ya Mandela, ghafla jambazi mmoja akamkaba Afisa Masoko, Bw. Mohamed Hossein Mompe, 35, wakamnyang`anya begi la rangi ya khaki lililokuwa na fedha hizo.

Akasema baada ya hapo wakawafunga kamba mikononi na miguuni, wakawekea plasta midomoni kabla ya kuwatupa na kukatokomea na pesa hizo.

``Hadi sasa tunaendelea kuwasaka watuhumiwa,`` akasema.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.