05 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mama Jijini Dar adaiwa kuua kwa kumtupa mwanae chooni
 
2009-05-05 20:46:38
Na Mwanaidi Swedi, Jijini

Mwili wa mtoto mchanga wa kike anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi saba umeokotwa ukiwa ndani ya shimo la choo pale Ukonga Mombasa Jijini Dar es Salaam.

Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Aibula Tanda, amesema tukio hilo limetokea majira ya saa 12:00 jioni.

Kaimu Kamanda Tanda amesema kuwa mtoto huyo anadaiwa kutupwa na mwanamke mmoja ambaye amefahamika kwa jina moja la Bi. Suna.

Aidha, amesema kuwa mwanamke huyo anahisiwa kuwa ndiye aliyetupa mtoto huyo kwa kuwa alikuwa mjamzito na kwamba baada ya tukio hilo, ametowekea kusikojulikana.

Kaimu Kamanda amesema kuwa hadi sasa, wanaendelea kumsaka na akipatikana watamfikisha mahakamani.

Akasema kuwa mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Amana.

Wakati huo huo, mwili wa mwanaume mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja umeokotwa huku ukiwa na majeraha kadhaa katika maeneo ya mdomoni.

Kaimu Kamanda Tanda amesema kuwa mwili huo umeokotwa jana majira ya saa 1:15 asubuhi pale katika Mtaa wa Zanaki, karibu na mgahawa unaoitwa Hong Kong.

Amesema kuwa mwanaume huyo anakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 35 na 40.

Aidha, akasema inadaiwa kuwa jeraha hilo limesababishwa na kupigwa na kitu kizito kilichomfanya apoteze meno yake mawili kabla ya kufariki dunia.

Amesema sababu za kifo chake hakikuweza kufahamika mara moja na uchunguzi unaendelea kuhusiana na tukio hilo.

Mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Taifa Muhimbili.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.