05 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Zombe akwaa kisiki
 
2009-05-05 20:54:07
Na Kiyao Hoza, Mahakama Kuu

Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe, ambaye yeye na wenzake wanashtakiwa kwa mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, amekwaa kisiki katika ombi lake la kutaka kurudia utetezi wake.

Jaji Salum Massati anayesikiliza kesi hiyo amesema leo asubuhi kuwa ombi lake limekataliwa kwa sababu akitoa ruhusa kwa Zombe kurudia utetezi wake upya, na washtakiwa wengine nao watadai kupewa nafasi hiyo ya kujitetea kwa mara nyingine.

Aidha, Jaji Massati amefunga utetezi kwa washtakiwa saba ambao ni mshtakiwa namba moja Zombe na Ahmed Makele (3), Jane Andrew (5), Mohamed Mabula (7), Michael Shinza (9), Abeneth Saro (10) na Rajab Bakari (12).

Hata hivyo, amesema kuwa washtakiwa namba mbili ambao ni Christopher Bageni na mshtakiwa namba 13 ambaye ni Festus Wabisabi, wao wataleta shahidi mmoja kila mtu.

Jaji huyo ameiahirisha kesi hiyo hadi kesho ambapo mashahidi wa washtakiwa hao watatoa ushahidi wao.

Jana Zombe kupitia wakili wake Jerome Msemwa aliiomba mahakama hiyo kumpa ruhusa ya kupanda kizimbani na kujitetea upya mara baada ya mshtakiwa wa mwisho Koplo Festus Chenge kumaliza utetezi wake.

Hata hivyo, Wakili Majura Magafu anayewatetea washtakiwa Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula alipinga madai hayo kwa madai kwamba hawajajiandaa juu ya utetezi huo mpya.

Magafu akadai kuwa suala hilo ni la kisheria na si kucheza bali kuwa makini ili wasivuruge mwenendo wa kesi hiyo.

Awali shahidi wa kwanza wa Zombe, Mkuu wa Gereza la Ukonga, Kamishana Msaidizi wa Magereza (ACP) Samuel Nyakitine, alidai kwamba hana uhakika kama mihuri na saini zilizokuwa katika barua ya Zombe ni vya ofisi yake.

Katika kesi ya msingi, Zombe na wenzake 12 wanadaiwa kuwa Januari 14 mwaka 2006, huko Mbezi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, waliwaua wafanyabiashara wa madini Sabinus Chigumbi, Ephraimu Chigumbi, Mathias Lukombe na dereva taksi Juma Ndugu, wakidai kuwa ni majambazi.

Awali kesi hiyo ilikuwa inawakabili askari polisi 13, lakini watatu waliachiwa baada ya kuonekana kwamba hawana kesi ya kujibu, ambao ni Noel Leonard, Moris Nyangerela na Felix Frederic. Mmoja Lema amekufa.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa ni Zombe, ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Kontebo Jane Andew, Konstebo Emanuel Mabula, Konstebo Michael Shonza na Koplo Abeneth Salo, Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Wabisabi.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.