05 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Ni vilio tu!
 
2009-05-05 20:55:02
Na Emmanuel Lengwa na Moshi Lusonzo

Wakati hadi sasa taarifa rasmi juu ya idadi kamili ya watu waliopoteza maisha katika mlipuko wa mabomu uliotokea wiki iliyopita Jijini Dar es Salaam ni 23, baadhi ya wananchi wa maeneo ya Mbagala, wanadai kuwa idadi ya waliokufa ni kubwa zaidi na kwamba miili yao huenda imekwama kwenye tope la mto Kizinga.

Kadhalika madiwani wa kata za Mbagala na Mbagala Kuu wameonyesha wasiwasi wao wakidai kuwa, wana hofu kwamba watu kadhaa wakiwemo watoto ambao walitoweka tangu siku ya tukio hilo la mlipuko, wakawa wamefia kwenye mto huo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleimani Kova amesema hadi sasa jumla ya watoto 19 wakazi wa Mbagala, tangu siku ulipotokea mlipuko huo, hawajulikani waliko.

Kufuatia hofu hiyo, jana Baraza la Madiwani la Manispaa ya Temeke liliitisha kikao cha dharura kujadili hali hiyo.

Katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, ambapo ndipo lilipotokea tukio hilo, Bw. Anderson Charles alisema kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo watoto wengi waliozama ndani ya mto Kizinga na kuwa miili yao imekwama kwenye tope la mto huo.

Akasema kasi ya uokoaji inayoendelea kufanywa na wananchi kwa kushirikiana na Polisi ni ndogo, hivyo akaomba Jeshi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ, kufanya operesheni maalum kusaka miili ya watoto hao na kuiopoa mtoni.

Hoja ya Bw. Charles iliungwa mkono na Diwani wa Kata ya Mbagala, Bw. Peter Osoro aliyesema kuwa baada ya milipuko, watoto wengi walikimbia na kuingia mtoni, wakiwa na nia ya kuvuka mto Kizinga kwenda ng\'ambo maeneo ya Yombo.

Kwa mujibu wa diwani huyo, watoto wengi walizama mtoni katika maeneo ya Kingugi na Bugudadi mahali ambapo wengi wao walitaka kuvuka wakidhani maji ya mto ni machache, lakini wakajikuta wakizama kwenye tope na kupoteza maisha.

Aidha Bw. Osoro akasema kuwa hadi sasa kuna familia nyingi zinahaha kutafuta ndugu, jamaa pamoja na watoto wao, na hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kupeleka kikosi cha JWTZ kufanya operesheni maalum.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Bw. Steven Kongwa aliwahakikishia madiwani hao ambao wengi wao walikuwa wakibubujikwa machozi kuwa, juhudi kubwa za kuwasaidia wahanga wa tukio hilo zinaendelea na hivyo akawataka waheshimiwa madiwani wasiwe na huzuni sana.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Temeke, Bw. Jerome Bwanausi, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maafa hayo, alisema kamati yake iko imara na wahanga wote wanapewa misaada.

Akasema mazishi ya maiti zote za ajali hiyo yamegharimiwa na kamati ya maafa ya mkoa wa Dares Salaam ambayo iko chini ya Mkuu wa Mkoa, Bw. William Lukuvi.

Madiwani hao walimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kutembelea majeruhi na wahanga wa tukio hilo.

Aidha waliwashukuru watu wote waliotoa misaada ya hali na mali kusaidia wahanga wa tukio hilo.

Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema kuwa watoto 19 ambao hawajulikani waliko wanahisiwa kuwa wamekimbilia maeneo mbalimbali na wengine wamehifadhiwa majumbani na wasamaria wema.

Ametoa wito kwa watu wanaowahifadhi watoto wasio wao majumbani au wale wanaojua walipo, watoe taarifa ili juhudi za kuwakutanisha na wazazi wao ziweze kufanyika.

``Kuna watoto wamekimbilia maeneo ya mbali, wapo waliofika hadi Arusha, lakini pia kuna wengine wamehifadhiwa na wasamaria wema, nawaomba wote wajitokeze kutoa taarifa zao ili tuwakutanishe na wazazi wao,`` akasema Kamanda Kova.

Ameonya kuwa miongoni mwa watoto hao wamo watoto wa kike na wanafunzi, hivyo kutotoa taarifa zao inaweza kuleta hisia mbaya baadaye na ikawa shida.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.