28 Apr 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Ukwapuaji kwenye nyumba za ibada udhibitiwe
 
2009-04-28 14:50:47
Na Beatrice Bandawe

Nyumba za ibada ni mahali patakatifu ambapo wafuasi wa dini mbalimbali huenda kumwabudu Mungu.

Ni mahala patakatifu ambapo kwa wafuasi halisi wa imani hiyo ni vigumu kufikiria kuwa muumini hasa anaweza kufanya uhalifu wa aina yoyote katika eneo hilo kwa sababu wanaamini kuwa jicho la Mungu linamuona na kuzisoma nyoyo za wafuasi wake.

Kwa wale waumini wa dini ya Kikristo siku zote ni za Mungu lakini siku ya Jumapili ni maalum kwa utukufu wake katika kumwabudu Mungu.

Na kwa waumini wa dini ya Kiislamu siku yao maalum ya utukufu ni Ijumaa licha ya siku zote kuwa na ibada za unyenyekevu kwa muumba.

Siku hizo kuu za kumtukuza Mungu, mara nyingi waumini wengi hujumuika kwa wingi pamoja ili kushirikiana katika swala na maombi.

Hata hivyo, kuna baadhi ya watu ambao yawezekana hujipenyeza katika mkusanyiko huo wakiwa na imani na msimamo tofauti.Yawezekana hupenyezwa na shetani au nguvu nyingine za giza.

Kwa hiyo badala ya kushiriki kuomba kwa unyenyekevu mkubwa na kuunyenyua utukufu wa Mungu, wao huwa mahodari kukwapua vitu vya thamani vya waumini halisi zikiwemo simu za mikononi, mikoba, fedha, viatu na vitu vinginevyo ambavyo huchukulika kwa urahisi wakati watu wamezama katika maombi.

Hivi karibuni Wakristo nchini kote walijumuika na wenzao wa duniani wote katika kusherehekea Siku kuu ya Pasaka ambayo ni kumbukumbu ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo.

Tukio hilo kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu lilivutia watu wengi kwenda kanisani kujumuika na wenzao.

Kwa desturi iliyozoeleka waumini wa dini ya Kikristo, baada ya mahubiri na kisha kuinuka kwenda kumtolea Mungu sadaka na shukrani kwa kubarikiwa.

Hutolewa katika vyombo maalum mara nyingi vinakuwa sehemu ya mbele ndani ya kanisa au kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya kanisa.

Kwa baadhi ya makanisa, wazee wa kanisa hupitisha vikapu au visanduku vidogo ambavyo waumini huweka sadaka zao.

Utaratibu wa makanisa mengine waumini kwenda mbele kutoa sadaka na kurudi sehemu zao walizoketi ndizo ambazo zimekuwa zikitumiwa kikamilifu na watu hao wasiomuogopa Mungu hata chembe kukwapua .

Kwa sababu ya unyeti wa eneo hilo kiimani, watu wote wanaaminiana na hivyo watu wanapokwenda mbele huacha vitu vyao kama mapochi, simu na vitabu bila kuwa na wasiwasi wowote.

Katika hali hiyo, siku hiyo ya Pasaka, mtu mmoja haileweki kuwa alitumwa na sheteni au nani alijipenyeza katika `joho` la muumini wa kanisa eneo la Mwananyamala Komakoma.

Wakati wa kutoa sadaka ulipofika alikwapua pochi ya muumini mmoja pamoja na simu ya muumini mwingine na kutokomea kusikojulikana.

Wakati tukio hilo likitokea , muumini mmoja alifunuliwa kiimani akamuona muumini huyo `feki` akiwa katika harakati hizo, lakini alinyamaza kwa kudhani pengine ameagizwa na muhusika kuchukua vitu hivyo.

Waumini waliporudi kuketi sehemu zao na kugundua pochi na simu zimetoweka, ndipo ilibainika kuwa mtu huyo ni mkwapuzi.

Kitendo hicho kiliwasikitisha wengi na kumfanya Padre wa kanisa hilo kuwatahadharisha waumini siku ya Jumapili kuwa wanapokwenda kutoa sadaka wasiache mapochi au simu zao ili kujinusuru na wakwapuzi wanaokwenda kwenye nyumba za ibada kukwapua.

Ni muhimu sana tabia hiyo ikadhibitiwa haraka waumini kwa kushirikiana na kuwafichua bila ya kusita ili wasivuruge utulivu wa maeneo hayo na mtiririko wa maombi yao kwa hofu ya kukwapuliwa.

Imewahi kulalamikiwa kuwa vitendo hivyo vya wizi pia vimekuwa vikijitokeza katika baadhi ya nyumba za ibada za waumini wa dini na madhehebu mengine, wakati waumini wanapovua viatu vyao na kuingia ndani kuabudu.

Watu wasiokuwa waaminifu huvikusanya viatu hivyo na kuondoka navyo.

Wakwapuzi wengine huthubutu hata kufungua milango ya magari ya waumini na kukwapua vitu vya thamani kama kompyuta na fedha.

Nyendo hizo hazifai.Huku ni kumtukuza shetani. Nyumba za ibada ni sehemu takatifu na unapofanya uhalifu wa aina yoyote unajihakikishia laana.

Inakuaje mtu unatoka nyumbani kwako na kupanga kwenda kwenye nyumba ya ibada na kuiba?

Kama una shida kwa nini usimweleze Padre au Sheikh pembeni kuwa unakabiliwa na tatizo fulani ili aweze kukuombea kwa waumini wenzio wakuchangie badala ya kujidhalilisha na kujitafutia laana.

Baadhi ya wadokozi hudiriki kuingiza mikono kwenye masanduku ya sadaka kudokoa fedha zinazotolewa. Wengine wanaoaminiwa kuhesabu sadaka hushawishika na kuchomoa.

Beatrice Bandawe ni Mhariri wa Habari wa Nipashe Jumapili.Anapatikana kwa simu 0713 466571 email [email protected]

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.