29 Apr 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

BoT izidi kumulikwa
 
2009-04-29 13:31:15
Na Mhariri

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, juzi alitangaza ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma katika kipindi cha mwaka 2007/08 iliyobainisha ufisadi mwingine katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Utouh alisema ukaguzi uliofanywa na ofisi yake kuhusu mkataba wa bima wa ujenzi wa majengo pacha katika makao makuu ya BoT unaacha maswali mengi kutokana na kuwa na mapungufu kadhaa.

Baadhi ya mapungufu aliyoyataja ni pamoja na kukosekana kwa dhamana ya bima, gharama za bima zilizolipwa kuonekana zimezidi kiwango, kuingia mikataba miwili inayofanana na kuwepo kwa taarifa zinazokinzana kwenye mkataba wa bima wa awamu ya pili.

Aliwaambia waandishi wa habari wakati akitangaza ripoti hiyo mjini Dodoma kuwa ameiomba Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa (Takukuru) kuchunguza mashaka yaliyomo kwenye mkataba wa bima wa ujenzi wa maghorofa hayo na kuchukua hatua stahili.

Alisema kati ya premiums za Dola za Marekani 6,302,823.42 zilizolipwa kwa wakala kati ya Februari 20, 2003 hadi Julai 24 2007, benki imeweza kupata dhamana zenye thamani ya Dola za Marekani 2,478,388 pekee na kuacha sehemu kubwa ya bima hizo kutokuwa na dhamana, badala yake benki ina barua tu kutoka kwa wakala.

Tatizo lingine alisema ni lile la benki kuingia mikataba miwili inayofanana, mmoja ukiwa umeingiwa na mkandarasi kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi, lakini benki baadaye ikalipa fedha kwa ajili ya bima hiyo hiyo.

Ripoti ya CAG inatoa tafsiri kubwa kuwa licha ya hatua mbalimbali ambazo serikali imekuwa ikichukua kupambana na ufisadi, bado kuna vitendo vikubwa na vya kutisha vya ufisadi katika mashirika yetu nyeti kama BoT.

Itakumbukwa kuwa BoT imeshakumbwa na kashfa kadhaa za ufisadi na kuwahusisha maofisa wake kadhaa ya kwanza, ikiwahusisha maofisa wanne katika wizi wa Sh, bilioni 133 uliofanywa na makampuni hewa 22 katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

Kashfa ya pili ni hasara ya zaidi ya Sh.bilioni 220 katika mradi wa ujenzi wa majengo pacha.

Tunampongeza CAG kutokana na kazi nzuri ya ukaguzi wa fedha za umma na kutoa mapendekezo ambayo yana lengo la kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za walipakodi.

Tunasema hivyo kutokana na kusikia kauli yake kuwa suala hilo amelifikisha Takukuru.

Ni aibu na fedheha kubwa kusikia vitendo vya ufisadi vikifanyika katika taasisi nyeti ya umma kama BoT, ambayo ina dhamana ya kusimamia uchumi wa nchi na fedha.

Taasisi kama hiyo inapogubikwa na ufisadi ni ndoto kupatikana kwa maendeleo ya kiuchumi.

Ripoti ya CAG ni changamoto kubwa kwa serikali. Jukumu lililoko mbele ya serikali ni kuifanyia kazi ripoti hiyo kwa kuchukua hatua zitakazobainisha ni kina nani walihusika katika kashfa hiyo na kuwafikisha mbele ya sheria.

Matukio haya yote yanatoa picha kwamba iliyokuwa bodi ya BoT wakati ule haikuwajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yake kama chombo cha kusimamia utendaji wa taasisi hiyo.

Haiingi akilini kusikia kwamba watendaji katika taasisi kama BoT wakaamua kufanya utekelezaji wa mambo makubwa kama kuingia mikataba na makampuni ya bima bila bodi kujua!

Je, wale waliokuwa wajumbe wa bodi hiyo wamechukuliwa hatua zipi kama njia ya kuwajibika kutokana na kupotea kwa fedha za walipa kodi?

Ni matumaini yetu kuwa serikali itatekeleza jukumu hilo hasakwa kuzingatia kauli ya CAG kuwa hatua yake ya kuiomba Takukuru kuchungua ni kuanza utekelezaji wa ushauri wa Rais Jakaya Kikwete ambaye aliitaka ofisi ya CAG, kushirikiana na vyombo vyenye mamlaka ya kuchunguza uhalifu kama vile polisi na Takukuru, pale inapogundua tatizo kubwa linaloashiria jinai katika pesa za walipa kodi.

Tunasubiri kuona hatua zitakazochukuliwa na dola ili kurejesha heshima ya taasisi hiyo nyeti mbele ya jamii na kwa maendeleo ya taifa letu.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.