01 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Hali ya kambi ya kuhifadhi waathirika
 
2009-05-01 14:22:59
Na Waandishi Wetu

Nako katika kambi za kuhifadhi watu waliopoteza makazi, Shirika la Msalaba Mwekundu, hadi jana lilikuwa likiendelea kutoa huduma kwa watu hao.

Shule ya msingi ya Kibaha English Medium kwa kushirikiana na Diwani wa Jangwani, walitoa msaada wa vyakula vyenye thamani ya Sh. milioni 2 kwa waathirika.

Diwani wa Mbagala, Tito Osolo, alisema jana kuwa eneo la Mbagala lina wakazi zaidi ya 120,000, zikiwamo kaya 7,000.

Hadi kufikia jana asubuhi watu waliopoteza makazi, mali zao na ndugu waliojitokeza kujiandikisha majina walifikia 500.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, aliwaambia waandishi wa habari katika kambi ya wagonjwa wa kipindupindu eneo la Hospitali ya Temeke ambako baadhi ya majeruhi wamelazwa, kuwa watu waliolazwa katika Hospitali ya Amana ni watano kati yao mmoja aliruhusiwa.

Alisema katika Hospitali ya Temeke walifikishwa wagonjwa 209, lakini hadi jana asubuhi walikuwa wamebaki wagonjwa 38 tu baada ya wengine kutibiwa na kuruhusiwa.

Afisa Uhusiano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Almas Jumaa, alisema wamepokea wagonjwa 26, wakiwamo wawili waliolazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Jumaa alisema kati ya wagonjwa hao, mmoja alipasuka sehemu ya kichwa na mwingine mguu ulikatika.

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali yaTemeke, Dk. Aisha Mahita, alisema hali za wagonjwa zinaendelea vizuri.

Aliishukuru Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Hospitali ya Aga Khan, Shirika la Msalaba Mwekundu na madaktari wa JWTZ kutoka Lugalo kwa kuwasaidia waathirika.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, alisema watapita katika kila nyumba kuandikisha majina ya watu wote waliopata hasara na mali zilizopotea na kwamba, wote watalipwa, hivyo akawataka kuondoa wasiwasi.

``Wote waliokosa makazi, zipo kambi mbili zimetengwa za kuwatunza. Huko serikali itawapatia chakula na malazi,`` alisema Lukuvi.

Alisema kama kuna watu wanaohitaji kuwachukua ndugu zao kwa ajili ya kukaa nao, wanaruhusiwa.

``Ila wasidhani kama malipo yao hayatakuwapo, malipo yao yako palepale,`` alisema Lukuvi na kuwataka waliopoteza ndugu, mali kujitokeza kujiandikisha majina.

Kuhusu fidia kwa makazi ya watu yaliyopotea, Lukuvi alisema hajafahamu vema, lakini akasema zimeundwa tume mbili za kuchunguza.

Alisema tume ya kwanza imeundwa kwa ajili ya kuandaa mazishi ya waliokufa, ambayo yatagharamiwa na serikali na kuongeza kuwa askari waliokufa watazikwa kwa heshima zote za kijeshi.

Lukuvi alisema tume hiyo inaongozwa na Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Jerome Bwanausi.

Alisema tume ya pili, inatokana na Kamati ya Jeshi ambayo itafanya tathmini ya wakazi wanaoishi karibu na kambi ya jeshi.

Alisisitiza kuwa kwa sasa hali ni shwari kwani hata Rais Kikwete aliweza kufika eneo la tukio na kushuhudia hali halisi iliyokuwapo.

``Tunaomba wananchi waondoe hofu,`` alisema Lukuvi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Msalaba Mwekundu Dar es Salaam, Mayasa alisema kambi zilizotengwa kwa ajili ya kuwatunza waliopoteza makazi na kupotea makwao, ni mbili; moja iko Mbagala Kizuiani na nyingine JKT Mgulani.

Alisema kati ya watoto 1,169 waliohifadhiwa, 384 wametambuliwa na waliopo hivi sasa ni 785 na kwamba, hadi kufikia jana watu wa jinsi hiyo walikuwa wakiendelea kupelekwa kwenye kambi hizo.

Imeandaliwa na Muhibu Said, Romana Mallya na Beatrice Shayo.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.