03 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Harusi inapovunjika dakika za mwisho
 
2009-05-03 18:59:53
Na Anti Flora Wingia

Zipo harusi zingine ukisimuliwa mikasa yake utadhani ni sinema za kuigiza. Pilikapilika nyingi tokea uchumba, maandalizi ya harusi zenyewe lakini katika kuhitimisha ndoa hazifungwi. Kulikoni?

Hivi majuzi nilikuwa sehemu katika kikao fulani cha harusi. Ni eneo linalotizamana na barabara kubwa iendayo Bagamoyo. Kabla ya kikao, ukapita msafara ambao tulidokezwa kuwa ni wa Kitchen Party.

Kitchen Party ni tafrija ndogo inayotangulia send-off kisha baadaye harusi. Tafrija hiyo inalenga kumfunda bibi harusi mtarajiwa kabla ya kuanza maisha ya ndoa na mumewe.

Naam. Mimi nikasema, ``hayo ni maandalizi ya harusi bila shaka…siku hizi upo msemo kwamba wanaooa au kuolewa miaka hii wanapeleka matatizo nyumbani``.

Baba mmoja aliyeketi pamoja nami akadakiza; ``umesema ukweli, harusi za siku hizi si lolote si chochote, gharama kibao lakini muda si mrefu wanaachana``.

Baba mwingine bila kuchelea akasema, “Ngoja niwasimulie ndoa moja iliyovunjika dakika za mwisho na kuacha wengi midomo wazi.

Ilihusu jamaa yangu mmoja.
Katika simulizi yake akasema kuwa yupo kaka mmoja ambaye ni jamaa yake alipania kumuoa mwanamama fulani. Maandalizi yakafanyika kuanzia kitchen Party, na send-off vyote vikafanyika.

``Maandalizi ya harusi yenyewe yaligharimu shilingi milioni 18,`` kwa mujibu wa baba huyu. Kila kitu kikawa tayari ikabakia kwenda kanisani ili ndoa ifungwe.

Siku ya harusi, bibi harusi akapelekwa saluni kutengenezwa na kuvalishwa. Bwana harusi naye akapelekwa kuandaliwa. Wageni waalikwa, ndugu na marafiki wakawahi kanisani.

Alivyoeleza baba yule ni kwamba muda wa kwenda kanisani ulipokaribia, ilitakiwa bwana harusi na mpambe wake waenda kumfuata bibi harusi ili kwa pamoja waweze kwenda kanisani.

Lakini ajabu ni kwamba bwana harusi alijaribu kumsaka aliko mkewe mtarajiwa bila mafanikio.

Walipokwenda saluni alikopambiwa aliambiwa kuwa yuko jamaa aliyekuja kumchukua na gari lililokuwa limepambwa vilivyo.

Kule kanisani wageni waalikwa pamoja na mtumishi wa Mungu aliyejiandaa kufungisha ndoa ile wakawa wanasubiri kwa muda mrefu wasijue kilichotokea.

Mwishoni wote wakakata tamaa na kutawanyika kurejea kwenye sherehe za harusi kujua kulikoni.

Kumbe baadaye akabainika kuwa yule jamaa aliyekwenda kumchukua bibie pale saluni alikuwa mpenzi wake wa zamani na hivyo kwa pamoja walitorokea kusikojulikana. Inaonekana bibi alikuwa anampenda aliyemtorosha kuliko yule waliyetaka kufunga ndoa naye.

Swali ni je, kwanini mwanamama huyu hakuwa wazi mapema kwa kueleza bayana kwamba bwana harusi yule mtarajiwa hakumpenda bali alikuwa na mwandani wake mwingine?

Hiyo ingesaidia mambo mengi pamoja na kuzuia gharama za maandalizi, usumbufu wa watu waliochanga fedha zao, wakaenda hata kanisani lakini harusi haikufungwa. Ama kwa hakika Maisha Ndivyo Yalivyo.

Ndoa zingine ni vurugu tupu. Usione watu wamesimama mbele ya mashekhe au pale madhabahuni huku maneno mazuri yaliyojaa upendo na matumaini yakiwatoka vinywani. Wengine ni usanii mtupu kama siyo unafiki.

Katika nafsi zao bado wanawakumbuka wapenzi wao wa zamani. Pale altareni inakuwa ni kuthibitisha tu kwamba eti nao wameoa au wameolewa kwa kufunga ndoa takatifu. Kumbe wakishatoka pale, mawasiliano na wachuchu wa zamani yanaendelea kama kawaida.

Matokeo yake ndiyo hayo tunashuhudia kuchipuka kwa nyumba ndogo au wengine wakikufuru zaidi huachana na wenzi wao au kutafuta visingizio ili ndoa zivunjikie mbali.

Haya siyo maisha bali ni kuongeza majanga ya kifamilia. Nyumba moja inakushinda sembuse nyumba mbili au tatu? Sijui labda niseme `mwenye nguvu mpishe` lakini madhara yake hayako mbali.

Msomaji wangu nikuachie nawe uchangie mawazo tuweze kusonga mbele kwa pamoja. Kama unacho kisa unadhani tunaweza kujadili kwa pamoja usisite kuniandikia kupitia email hii hapa chini.

[email protected]
Wasalaam

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.