04 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Vita ya Ligi Kuu haikuwa ya ubingwa bali...
 
2009-05-04 16:45:18
Na Adam Fungamwango

Ligi ya soka Tanzania Bara 2008/9, ilimalizika wiki iliyopita na kushusha pumzi ya mashabiki wa soka ambao roho zao zilikuwa juu kwa msimu mzima.

Mashabiki wengi wa soka waliohojiwa walisema kuwa ligi ya mwaka huu ilikuwa na msisimko wa aina yake, kuliko nyingine za miaka michache iliyopita.

Ligi hiyo imemalizika kwa Yanga kutetea ubingwa wake wa mwaka jana, ambapo mwaka huu imeupata kirahisi zaidi kwa kushinda mechi nyingi na idadi kubwa ya mabao katika raundi ya kwanza, kitu kilichowapa urahisi katika raundi ya pili, ambapo haikutumia nguvu kubwa kuupata.

Hayo pia yamethibitishwa na mashabiki ambao wamesema kuwa utamu wa ligi ya mwaka huu haukuwa kwenye kutafuta ubingwa kwa sababu alijulikana wazi, ila ilikuwa ni kutafuta nafasi ya kuwakilisha nchi katika kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF) pamoja na vita ya kupigania kutoshuka daraja.

Vita hizo mbili, zilifunika kabisa ubingwa wa mwaka huu kama vile hauna thamani, ambapo kupata nafasi ya pili na kubaki ligi kuu kilikuwa kitu cha thamani kubwa, na kuwa midomoni mwa mashabiki wengi wa soka.

Cha ajabu hata Yanga wenyewe wakiwemo viongozi wao, wakaacha kuuzumngumzia ubingwa wao, na wao wakajikita huko huko kwenye vita ya wenzao kutafuta nafasi ya pili.

Baada ya Simba, Kagera Sugar, Mtibwa, Prisons na JKT Ruvu kupigana vikumbo kwa muda mrefu kutafuta nafasi hiyo, mwishowe Simba na Mtibwa ziliziengua timu nyingine na wao kuingia kwenye vita hiyo hadi mwisho wa ligi ambapo Simba ilifanikiwa kutwaa nafasi hiyo.

Ushahidi wa hilo unajionyesha pale mashabiki wa Simba waliposhangilia kupita kiasi kupata nafasi ya pili walipoifunga Polisi Dodoma mabao 2-0, lakini mashabiki wa Yanga hawakuonekana kushangilia wakati timu yao ilipokabidhiwa kombe la ubingwa, hii yote inatokana na kuwa msisimko wa ligi ya mwaka huu ulikuwa kwenye maeneo hayo mawili tu.

Timu ya Polisi Moro hatimaye nayo ilishuka kwa mbinde baada ya kupigana hadi dakika za mwisho ikizing\'ang\'ania kooni, Moro United, na Toto Africa, lakini siku ya mwisho iliungana na Polisi Dodoma na Villa Squad. Zifuatazo ni takwimu mbalimbali za ligi ya mwaka huu jinsi ilivyokuwa.


Magoli
Jumla ya magoli 315 yamefungwa kwenye ligi ya msimu huu katika mechi 131 zilizochezwa, magoli 153 yakifungwa kwenye raundi ya kwanza na 162 yakifungwa katika raundi ya pili.

Magoli hayo yamefungwa na wachezaji 125, ambao ni baadhi tu ya wachezaji walioshiriki ligi huku, 29 yakifungwa kwa mikwaju ya penati na matatu yakiwa ya wachezaji kujifunga wenyewe.

Penati
Kwenye ligi ya mwaka huu, jumla ya penati 38 zimetolewa na waamuzi, ambapo katika hizo 29 zimetinga nyavuni na tisa kuota mbawa kwa kudakwa na makipa au kutoka nje.

Timu ya Simba ndiyo inaonekana kuongoza kwa kupewa penati nyingi, ambapo imezawadiwa penati sita, ikifuatiwa na Yanga pamoja na Prisons kila mmoja wakipata penati tano na Azam ikiwa na penati nne.

Mchezaji wa Prisons, Suma Addo ameongoza kwa ufungaji wa magoli ya penati akiwa amefunga magoli matano, akifuatiwa na Boniface Ambani wa Yanga akiwa amefunga manne pamoja na Shekhan Rashid wa Azam, huku Orji Obina na Mussa Hassan Mgosi wa Simba wakiwa wamefunga magoli matatu kila mmoja.

Wachezaji ambao wamekosa penati kwenye ligi hii ni Godfrey Taita na Laurent Mugia wa Azam, Filipo Alando wa Azam (wakati yuko Kagera), Thomas Mourice wa Moro United, Rashid Roshwa na Ramadhani Shamte wa Toto, Nurdin Bakari wa Yanga, Shaaban Kisiga na Osbone Manday wa Azam.

Goli la kwanza na la mwisho ligi kuu Emeh Izuchukwu wa Simba ndiye mchezaji wa kwanza kufunga goli kwenye ligi ya mwaka huu, alipofunga goli katika dakika ya 27 kwenye mechi kati ya timu yake na Villa Squad Agosti 22 mwaka jana kwenye mechi za ufunguzi ambapo Simba ilishinda magoli 4-1.

Magoli mengine katika mechi zote za ufunguzi yalifungwa baada ya dakika hiyo kupita.
Pia mchezaji Chesido Mathew wa Villa Squad ndiye aliyefunga goli la mwisho la kufunga ligi hiyo, kwenye ushindi wa mabao 5-4 dhidi ya Yanga, alilolifunga katika dakika ya 81.

Ikumbukwe kuwa Chesido pia ndiye aliyefunga goli la kufutia machozi kwa Villa siku Simba ikishinda kwa mabao 4-1 kwenye mechi ya ufunguzi wa ligi ambayo Izuchukwu aliweka rekodi ya kufunga bao la kwanza msimu huu.
Goli la mapema zaidi na la dakika za mwisho.

Rekodi ya goli lililofungwa mapema zaidi kwenye ligi ya msimu huu inashikiliwa na Nizzar Khalfan wa Moro United ambaye alifunga goli katika sekunde ya 29 tu ya mchezo wakati timu yake ilipocheza na Polisi Dodoma, akivunja rekodi zilizowekwa na akina Omari Matuta wa Mtibwa sekunde ya 57, Ambani na Hussein Bunu wa JKT Ruvu dakika ya kwanza, Meck Mexime wa Mtibwa dakika ya pili, Selemani Batili wa Polisi Dodoma dakika ya nne, Ambani tena dakika ya sita na Mgosi dakika ya 14.

Wachezaji wanne wanashikilia rekodi ya kufunga magoli katika dakika za majeruhi nao ni Lameck Dyton wa Villa Squad, Mussa Kipao na Shekhan Rashid wa Azam, Davis Naftari wa Simba na Jerry Tegete wa Yanga.

Shekhan alifunga goli la penati dhidi ya Simba katika dakika za majeruhi na kuifanya timu yake iondoke na ushindi wa magoli 2-0 mechi ya mzunguko wa kwanza, Naftari aliifungia Simba bao la pili na la ushindi dhidi ya polisi Moro na

kuifanya ishinde mabao 2-1 katika raundi ya kwanza mjini Morogoro, Tegete aliisawazishia Yanga dhidi ya Simba na kufanya timu hizo zitoke sare ya mabao 2-2.
Magoli ya kujifunga.

Wachezaji Shaaban Aboma wa Toto Africa, Lackson Kakolaki wa Azam na David Mwantika wa Prisons ndiyo waliosababisha ligi hiyo kuwa na magoli matatu ya kujifunga.

Aboma alijifunga wakati timu yake inapambana na Polisi Morogoro, Kakolaki alijifunga kwenye mechi kati ya timu yake na Villa Squad na Mwantika alijifunga kwenye mechi ya mwisho wa ligi kati ya Prisons na Moro united, bao lililoisaidia Moro kushinda mabao 2-1 na kunusurika kushuka daraja.

Wafungaji bora
Ambani ndiye ametwaa kiatu cha dhahabu kwa kufunga magoli 18, akifuatiwa na Bunu ambaye amemaliza akiwa na magoli 13, Benald Mwalala wa Yanga yeye amepata magoli manane, Said Dilunga wa Toto, Addo wa Prisons na Thomas Mourice wa Moro Unite wakiwa na magoli saba kila mmoja.

Wachezaji Obina, Mgosi, Nicolaus Kabipe wa Polisi Moro, Nsa Job wa Azam, Selemani Kibuta wa Moro United na Admin Banti wa Polisi Dodoma wao wamemaliza ligi kwa kufunga magoli sita kila mmoja.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.