06 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Zombe asubiri hukumu
 
2009-05-06 20:03:27
Na Waandishi Wetu

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imefunga utetezi wa mshitakiwa wa kwanza aliyekuwa Kaimu Kamanda na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, (ACP) Abdallah Zombe, kwenye kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, sasa anachosubiri ni hukumu.

Zombe kupitia wakili wake, Jerome Msemwa, juzi aliiomba mahakama hiyo impe nafasi ya kujitetea upya lakini ombi lake liligonga mwamba jana.

Mbali na Zombe washitakiwa wengine ambao utetezi wao umefungwa baada ya kuwasilisha ushahidi wao, ni mshitakiwa wa tatu, Ahmed Makelle, watano Jane Andrew, wa saba Emmanuel Mabula, wa tisa Michael Chonza, wa 10 Abeneth Saro na wa 12 Rajabu Hamisi.

Washitakiwa ambao utetezi wao haujafungwa ni wawili, Christopher Bagen, ambaye ni mshitakiwa wa pili na Festus Chenge mshtakiwa wa 13, ambao leo wataleta mashahidi wao mahakamani hapo.

Washitakiwa wengine waliiambia mahakama hiyo kuwa hawana mashahidi na hivyo utetezi wao ulifungwa.

Awali, Zombe alitaka kutoa tena ushahidi wa namna ambavyo barua anazodai ziliandikwa na washitakiwa wenzake na zikatoka gerezani kinyume cha utaratibu kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP).

Zombe anadai kuwa barua hizo zilizopelekwa kwa DPP na washitakiwa wenzake ndizo zilisababisha afunguliwe mashitaka hayo yanayomkabili. Akitoa uamuzi kuhusu ombi la Zombe la kujitetea upya, Jaji Salum Massati wa Mahakama ya Rufani, alisema hakuna sababu za msingi ambazo zinaweza kuishawishi mahakama kumruhusu Zombe kusimama kujitetea kwa mara ya pili.

Jaji Massati ambaye alianza kusikiliza kesi hiyo akiwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu kabla ya kupanda na kuwa wa Mahakama ya Rufani, alisema katika maombi yake (Zombe) hakuonyesha kama kuna kitu kipya ambacho atakiongelea ambacho hakifanani kabisa na utetezi aliokwishautoa.

Jaji huyo ana kibali cha Jaji Mkuu cha kuendelea kusikiliza kesi hiyo ambayo tangu ianze kunguruma Mahakama Kuu Machi mwaka jana imevuta hisia za watu wengi na idadi kubwa ya watu wanafurika kuisikiliza.

Jaji Massati alisema mahakama imeona endapo Zombe atapewa nafasi ya kujitetea anaweza kuwagusa washitakiwa wengine ambao nao itabidi mahakama iwaruhusu kufanya hivyo, jambo ambalo linaweza kuvuruga mwenendo mzima wa kesi hiyo.

Alisema Sheria ya Ushahidi namba 147, kifungu cha (4) kinaipa ruhusa mahakama kumruhusu mshitakiwa kujitetea upya iwapo tu itajiridhisha kuwa utetezi atakaoutoa hautaathiri mwenendo wa kesi na kuwagusa washitakiwa wengine.

Endapo mshitakiwa wa pili na wa 13 wataleta mashahidi wao leo na kumaliza ushahidi wao, kesi hiyo itakuwa imefikia ukingoni ambapo Jaji Massati atakuwa na kazi ya kuandika hukumu.

Awali, wakati upande wa mashitaka unafunga ushahidi wake, Zombe aliiambia mahakama hiyo kuwa anatarajia kuleta mashahidi saba, lakini hakufanya hivyo na sababu za kutowaleta hazijajulikana.

Mbali na Zombe washitakiwa wengine ni Christopher Bageni, Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Chonza, Abeneth Saro, Rajabu Hamis na Festus Chenge.

Katika kesi hiyo, washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka manne ya mauaji.Wanadaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, Ephraimu Chigumbi, Mathias Lukombe na dereva teksi Juma Ndugu.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.