|
Walimu wapya Rombo hawajapata mishahara yao
2009-05-07 11:49:42
Na Richard Makore
Wilaya ya Rombo ,mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo yaliyofanikiwa sana kielimu hapa nchini lakini bado kuna changamoto mbalimbali zinazotakiwa kutatuliwa ili kuwafanya walimu wafanye kazi katika mazingira mazuri.
Mwandishi Wetu anafafanua katika makala hii kama alivyozungumza na watendaji wa serikali, walimu na wanafunzi wilayani humo.
UKIPITA katika baadhi ya maeneo wilayani Rombo utaona shule nyingi zikiwemo za msingi na sekondari zikiwa zimejengwa vizuri.
Shule hizo zina walimu waliohitimu mafunzo yao vilivyo na wamepelekwa huko na serikali ili kuweza kufundisha shule mbalimbali.
Hata hivyo pamoja na hali hiyo nzuri kuna changamoto kadhaa zinazowakabili walimu hasa wale wanaoanza kazi hivi sasa na wale walioajiriwa kuanzia miaka miwili iliyopita.
Walimu waliozungumza wilayani humo wanasema,serikali imewasahau na hivyo kushindwa kuwalipa mishahara ingawa wameajiriwa kwa mujibu wa sheria za utumishi wa serikali.
Mwalimu Undiri Yohana kutoka shule ya Sekondari ya Kelamfua iliyopo katika kijiji cha Kelamfua anasema, walimu wanaopata shida zaidi ni wale wanaofundishwa katika shule za kata.
Shule hizo anasema licha ya kujengwa vizuri lakini wao kama watumishi wahazifurahii kwa sababu serikali inawafanyisha kazi bila malipo na kwamba hakuna mtu anayejitokeza na kutoa majibu ya matatizo yanayowakabili.
Anasema pengine serikali inafanya makusudi kutowalipa malimbikizo mbalimbali wanayoidai jambo ambalo linawafanya kuishi katika maisha magumu.
Mwalimu mwingine Regina Kavishe anasema, walimu wa shule za msingi wana unafuu zaidi kuliko wale wanaofundisha sekondari kwa sababu wao Chama cha Walimu (CWT) kinawatetea na kuwafanya wapate haki zao mapema.
Kutokana na kutopata mishahara kwa muda mrefu baadhi ya walimu, wanalazimika kuendelea kuwategemea wazazi kuwapatia fedha za matumizi mengine pamoja na chakula.
Mwalimu Kavishe anasema, walimu wa kike ambao idadi yao ni kubwa ,ndilo kundi linaloteseka zaidi.
Anasema ni bora mwalimu kujitoa katika ualimu ambao hapati mshahara kwa wakati na kuamua kwenda kuanzisha genge la kuuza nyanya mtaani.
Naye Mwalimu Hedwigis Mrema anasema, suala la maslahi ya walimu limekaa kisiasa zaidi kuliko hali halisi ilivyo.
Hata hivyo anasema, kutokulipwa mshahara bado hakujaathiri sekta ya elimu katika wilaya hiyo iliyopakana na nchi ya Kenya.
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza wanawasifu walimu wao kwamba licha ya kukabiliwa na hali ngumu ya maisha bado hawajawahi kupata wazo la kuanza kufundisha masomo ya ziada maarufu kama tuition.
Wanaserma ujasiri huo unafaa kuigwa kwani kama walimu hao wangepata wazo la kufundisha masomo ya ziada wanafunzi wengi wasingemudu kulipa jambo ambalo lingeweza kushusha kiwango cha elimu.
Kaimu ofisa elimu wa Wilaya hiyo, Abel Nakazael anakiri kuwa walimu wanateseka kwa kutokulipwa mshahara wao kwa wakati.
``Moja ya matatizo yanayowakabili walimu ni pamoja kufanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kulipwa mshahara`` anasema.
Anasema matatizo mengine ni pamoja na walimu kukaa muda mrefu bila ya kupata mafunzo.
Anafafanua kwamba kutokana na wilaya hiyo kutokuwa na fedha za kuwapatia mafunzo, walimu hao wanalazimika kufundishana wenyewe kwa wenyewe katika masuala ambayo baadhi yao wanakuwa wana ujuzi zaidi kuliko wengine.
Nakazael hata hivyo anakataa kuwa ualimu sio wito bali ni kazi kama ilivyo kazi zingine ambayo mtu akifanya anahitaji kupata mshahara.
Kutokana na tatizo la walimu wapya kukaa muda mrefu bila kulipwa, kamati za shule kwa kushirikiana na Mkuu wa shule wanalazimika kutafuta fedha kwa ajili ya kumpa posho ya kuijikumu mwalimu anayeanza kazi.
Anasema shule inalazimika kutumia fedha za elimu ya uzalishji (EK) kumlipa mwalimu ili angalau kumvutia asikimbie na kuacha kazi hiyo.
Ofisa elimu (taaluma) katika Wilaya hiyo, Elibariki Mashangia anasema maisha ya walimu wanaoanza kazi ni mbaya zaidi kutokana na kutokulipwa mshahara.
Aidha, anasema walimu katika wilaya hiyo hapati huduma ya matibabu kupitia Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).
Kwa upande wa walimu, anasema wengi wao wanakimbia na kuacha kazi muda mfupi baada ya kuripoti katika vituo vyao vya kazi.
Anaongeza kuwa gharama ya kununua maji ndoo moja ya lita 20 inauzwa Sh. 500 na kwamba kwa mwalimu anayeanza kazi hawezi kumudu kuyanunua.
Anasema wakati wa kiangazi wananchi wengi wakiwemo walimu wanalazimika kuvuka mpaka na kuingia nchini Kenya kwa ajili ya kwenda kutafuta maji.
Mashingia alisema, wanyama aina ya punda ndiyo wanaotumika kubeba maji hayo ambayo ili kuyapata mwalimu analazimika kutumia zaidi ya saa nane kwenda na kurudi.
Anafafanua kuwa walimu waliopo mpakani mwa Kenya katika tarafa ya Tarakea ndiyo wana maisha magumu zaidi.
Aidha, kwa upande wa huduma za hospitali anasema baadhi ya walimu hawazipati licha ya kuwa wanakatwa bima ya afya.
Baadhi ya walimu waliozungumza na Nipashe katika shule ya msingi ya Kamwanga walikiri kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu.
Walisema huduma ya matibabu wanalazimika kuifuata nchini Kenya katika hospitali ya Laotokitoki.
``Tukienda Rombo katika hospitali ya Huruma hatupati huduma tunaambiwa bima ya afya hatuitambui licha ya kwamba kila mwezi tunakatwa fedha kwa ajili ya kuchangia mfuko wa bima ya afya``.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halamshauri ya Wilaya hiyo, Elias Mshana anakiri kuwa watumishi hao huvuka mpaka na kwenda kutafuta huduma hizo nchini Kenya
Anasema suala la walimu kutopata huduma ya afya kupitia mfuko wa bima ya afya ni la kiwizara na kwamba kuna magonjwa ambayo wanatibiwa lakini mengine hawatibiwi.
Anakiri walimu kukatwa fedha nyingi ajili ya kuchangia mfuko wa bima ya afya lakini haziwasaidii kupata huduma hiyo.
|