07 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Z`bar yaunda timu kukabiliana na homa ya mafua ya nguruwe
 
2009-05-07 15:25:59
Na Mwinyi Sadallah

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imeunda kamati ya kukabiliana na tatizo la homa ya mafua ya nguruwe, maradhi ambayo yameanza kuathiri baadhi ya mataifa zaidi ya 20 duniani kote.

Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, aliwaambia waandishi wa habari jana akiwa ofisini kwake Vuga.

Homa ya mafua ya nguruwe hadi sasa imeathiri zaidi mataifa ya Mexico na Marekani huku baadhi ya mataifa yakichukuwa hatua ya kuuwa nguruwe.

Nchi nyingine zilizoripotiwa kuwa na wagonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe ni Canada, Hong Kong, Costa Rica, Colombia, El Salvador, Israel, New Zealand, Korea, Hispania, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Austria, Denmark, Ireland, Uholanzi, Ureno na Uswsi.

Waziri Juma alisema kamati iliyokuwa ikisimmaia tatizo la homa ya mafua ya ndege ndio itakayochukuwa jukumu la kusimamia tatizo la homa ya mafua ya nguruwe, wakati wowote litakapojitokeza visiwani.

Waziri Hamza, alisema kamati hiyo ambayo ipo chini ya ofisi yake itafanya kazi kwa kushirikiana na wataalamu wa Wizara ya Afya na Mifugo.

Alisema watalaamu watahakikisha inakuwepo tahadhari kubwa kwa watu wanaoingia na kutoka nchini.

Alisema itakapotokea kuna mtu ama watu wana dalili za ugonjwa huo watangewa eneo la dharura.

Alisema Zanzibar inategemea sekta ya utalii kiuchumu, hivyo lazima wataalamu wa afya nchini kuchukuwa tahadhari mbali mbali, kwa vile ugonjwa huo unaonekana kuathiri mataifa mengi yakiwemo ya Ulaya.

Waziri huyo alisema Serikali inafahamu kuna watu wanaingia na nyama aina tofauti kutoka nje ya maeneo ya Zanzibar, hivyo ni vizuri wataalamu wa afya wakazifanyia ukaguzi nyama hizo ili kuepusha maradhi ya ugonjwa huo ama magonjwa mengine kuingia nchni.

Hata hivyo alisema Serikali haifikirii kupiga marufuku ufugaji wa nguruwe kwa vile hadi sasa maradhi hayo hayajathibitika Zanzibar.

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar, Dk. Kassim Gharib Juma, alisema kwamba kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2003 Zanzibar ina nguruwe takriban 535.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.