07 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Ujambazi warindima Dar, Arusha, Mwanza
 
2009-05-07 15:28:09
Na Waandishi Wetu Dar na Mikoani

Wimbi la matukio ya ujambazi wa kutumia silaha limeibuka kwa kasi katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Dar es Salaam ambako watu 11 wanaoshukiwa kuwa majambazi sugu wamenaswa na polisi huku mmoja akiuawa.

Huko Arusha majambazi saba akiwemo mwanajeshi mstaafu na polisi mstaafu, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo baada ya kukamatwa na bunduki mbili ambazo ni SMG yenye namba 2740 ikiwa na risasi 22 na magazine mbili pamoja na bunduki aina ya uzi namba 2238061 ikiwa na risasi 23.

Majina ya watuhumiwa hao wa ujambazi ni Joseph Elius (54) mkazi wa Karatu ambaye ni mstaafu wa Jeshi, Feruzy Hamisi (28) anayeishi Babati, Bruno Zakaria (27) wa Sanawari Manispaa ya Arusha na Athumani Said (42), mkazi wa Sepuko Singida.

Wengine ni Daniel Peter (48) mkazi wa NMC mjini Karatu, Wema Panga (30) wa Girambo Karatu na Mohamedi Juma (40) anayeishi Njiro, Arusha ambaye ni polisi na hakufahamika kama alifukuzwa au alistaafu kazi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Parmena Sumary, alisema majambazi hayo yalifanya uporaji maeneo mbalimbali ambapo Jumatatu wiki hii, saa 2.45 huko Kilimatembo wilayani Karatu, walimvamia dereva David Nyanguti Mwikoma (36) akiwa kwenye gari namba T 586 ACQ na kumpora fedha tasilimu Sh. 270,000 na simu ya kiganjani aina ya Nokia.

Sumary alisema baada ya kumpora pia walimpiga na kumjeruhi, kisha yakatokomea hadi mbele ya eneo hilo na kusimamisha gari la abiria aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili T 366AMK lililokuwa likitokea Arusha kwenda Karatu na kuwapora abiria waliokuwamo na kutokomea.

Alisema baada ya kufanya tukio hilo ambalo bado thamani ya vitu vilivyoibwa haijapatikana, majambazi hayo yalikwenda hadi kijiji cha Ayaramba Gugerna na kumvamia mzee mmoja, Qamara Tluway (65) na kumpora simu na fedha ambazo hazikutajwa.

Akielezea zaidi, Kamanda Sumary alisema baada ya kupora mali hizo, majambazi hayo yalifyatua risasi hewani ovyo na kujeruhi watu watatu ambao ni Israel Wamara (23), Pinda Wamara (26) na mwenzao Daniel Bura (32) na risasi nyingine ilimpiga ng’ombe na kumuua.

Alisema baada ya kufanya uhalifu huo yalikwenda porini kujificha hadi alfajiri ya juzi yalipolisimamisha gari aina ya Toyota Land Cruiser iliyokuwa ikitoka Karatu kwenda Arusha na kupanda.

Alisema baada ya kupanda gari hilo, polisi walipewa taarifa na raia wema na kulizuia gari hilo, kisha kufanikiwa kuwanasa wakiwa na silaha hizo na wanaendelea kuhojiwa na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.

Kwa upande wa Jiji la Mwanza Jeshi la Polisi mkoani humo linawashikilia watu wanne kwa tuhuma ya kukutwa na bunduki aina ya SMG pamoja na risasi 26.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Elias Kalinga, alisema watu hao walikamatwa Jumatatu wiki hii, saa 8:00 usiku katika Kijiji cha Katoro wilayani Geita.

Alisema watu hao walikamatwa kufuatia doria ya polisi iliyofanyika kutokana na matukio ya uvamizi kwenye nyumba nyakati za usiku kuongezeka.

Kalinga aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Hoja John (22) ambaye alikutwa nyumbani kwake akiwa na bunduki aina ya SMG yenye namba UA39701997 na risasi 26 akiwa amezihifadhi chumbani kwake.

Alisema alipohojiwa alidai kuwa ameuziwa na watu watatu kwa gharama ya Sh. 80,000 ambao aliwataja kuwa ni Night Damas (37), Kululinda Kasara (40) na Makisio Paranyange (21) ambapo polisi walifanikiwa kuwatia mbaroni.

Alisema watatu hao walipohojiwa walikiri kumuuzia bunduki na risasi mwenzao kwa madai kuwa waliikuta shambani ikiwa imefukiwa ardhini wakati walipokuwa wakilima.

Kalinga alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Katika Jiji la Dar es Salaam, mtu mmoja aliyetajwa kuwa jambazi sugu ameuawa jijini hapa katika mapambano na polisi waliokuwa doria.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, ilisema jambazi huyo, John Madiba (41), mkazi wa Arusha na Kitunda, Dar es Salaam, alifariki juzi saa 2:15 alipokuwa akipelekwa hospitali baada ya kujeruhiwa na risasi wakati wa mapambano.

Katika taarifa hiyo, Kamanda Kova alisema siku ya tukio, marehemu huyo akiwa na wenzake wawili walimpora mwanamke mmoja, Pamela Makame (39), gari aina ya Toyota Corolla na kukimbia nayo.

Alisema polisi waliokuwa doria walipata taarifa hizo na kuanza kuwasaka ambapo waliwakimbiza hadi Kinondoni.

Kova alisema majambazi walipozidiwa mbio na polisi, wawili walifanikiwa kutoroka na kwamba marehemu hakuweza kukimbia kutokana na majeraha ya risasi aliyokuwa nayo.

Katika taarifa hiyo, Kova alifafanua kuwa polisi walipekuwa gari hiyo na kumkuta jambazi huyo akiwa na bunduki moja aina ya SMG iliyokuwa na risasi 29.

Alisema katika tukio hilo, askari wa upelelezi namba D 8549 CPL Deogali alipata majeraha ya risasi katika goti lake la mguu wa kulia na kwamba anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Alisema polisi wanaendelea na msako ili kuwakamata majambazi waliotoroka.

Imeandaliwa na Cynthia Mwilolezi, Arusha; Grace Chilongola, Mwanza; na Restuta James, Dar.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.