07 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wanajeshi kulipua mabomu 75 leo
 
2009-05-07 15:29:28
Na Romana Mallya

Mabomu 75, dazeni kadhaa za viwashio pamoja na fyuzi zake zilizotokana na mlipuko wa mabomu yanatarajia kuharibiwa kwa kulipuliwa leo kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Mbagala jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alisema juna kuwa zoezi la kuyalipua masalia ya mabomu hayo litafanywa na wataalamu wa kikosi maalum cha uhandisi cha jeshi kuanzia saa 9:00 alasiri hadi saa 11:00 jioni.

Dk. Mwinyi alisema kikosi hicho kitafanya kazi hiyo kwa utaratibu wa kutanguliza milipuko miwili midogo kwa ajili ya kutoa tahadhari kwa wananchi kisha kuyalipua mabomu hayo.

Alisema baada ya milipuko hilo, itafuatiwa na milipuko mingine ya nguvu kiasi ambayo itakuwa ikilipuliwa kwa mfululizo hadi saa 11:00 jioni.

``Wananchi tunawaomba wakae umbali wa mita 500 kutoka eneo la milipuko kupisha zoezi hilo.

Wizara yangu inawahakikishia wananchi kazi hiyo itafanyika kwa uangalifu mkubwa na kwa usalama na hayatakuwa na sauti kubwa kama yale ya awali,`` alisema.

Alisema wananchi wasiwe na hofu kwani mita zilizowekwa ili wakae ni za kitaalamu na hayatakuwa na madhara kwao.

Kadhalika, Dk. Mwinyi alisema wameamua kuyaharibu mabomu hayo kwa kuyalipua kwani kiutaratibu bomu linapopata mtikisiko huwa haliwezi kuhamishika.

Aidha, Dk. Mwinyi alisema katika eneo hilo ili kusaidia kazi hiyo iende kama ilivyopangwa kutakuwa na wanajeshi ambao watakuwa wakiwaelekeza wananchi maeneo ya hatari ambayo hawatakiwi kukaa ili madhara mengine yasitokee tena.

Hata hivyo, Dk. Mwinyi alipotakiwa kutoa thamani ya mabomu hayo yanayoharibiwa leo, alisema hiyo ni mmoja ya kazi iliyopewa Baraza la Uchunguzi hivyo wananchi wawe na subira.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, alisema wakati zoezi hilo likiendelea kufanyika huduma zote za kijamii ziendelee kutolewa kwani milipuko hiyo haina madhara kwa wanadamu.

``Wananchi wanaoishi maeneo hayo wawaruhusu watoto wao kwenda mashuleni na huduma za hospitali na nyingine ziendelee, kwani milipuko ya kesho (leo) haitakuwa na madhara kama iliyopita,`` alisema.

Lukuvi alisema mabomu hayo yalipatikana kutoka kwenye shimo la kwanza kwenye kambi hilo ambayo yalishindwa kulipuka awali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama Jeshini, Brigedia Paul Mella, alisema zaidi ya wanajeshi 200 wamesambazwa eneo hilo ili kuhakikisha wananchi wanakaa mbali na hapo.

Mabomu yaliyolipuka hivi karibuni huko Mbagala, yameua au kusababisha vifo vya watu 25, huku yakiharibu zaidi ya nyumba 4,600. Serikali tayari imeanza mchakato wa kuhakiki nyumba zilizoathiriwa kwa lengo la kuwafidia waathirika.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.