07 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Zombe abubujikwa machozi
 
2009-05-07 15:30:57
Na Joseph Mwendapole

Mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, aliyekuwa Kaimu Kamanda na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe, jana alimwaga machozi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, sababu halisi ya Zombe kumwaga machozi haikueleweka ingawa wakili wake, Jerome Msemwa, alidai kuwa mteja wake ametoa machozi ya furaha baada ya kesi hiyo kufikia ukingoni na kwamba anasubiri hukumu.

Zombe alionekana mara kadhaa akijifuta machozi wakati shahidi wa mshitakiwa wa 13, Mori Nyangerera, akiendelea kutoa ushahidi dhidi ya Festus Chenge.

``Ni kweli mteja wangu ametoa machozi, lakini ni machozi ya furaha baada ya kuona kesi inafikia ukingoni na sasa anasubiri hukumu,`` alisema Msemwa.

Shahidi Nyangerera alidai kuwa Zombe aliwaita na kuwapa pongezi ofisini kwake siku moja baada ya tukio na kisha akaamuru wapandishwe vyeo baada ya kukamata wafanyabaishara waliodaiwa kuwa ni majambazi maeneo ya Sinza Palestine, jijini Dar es Salaam.

Jaji Salum Massati wa Mahakama ya Rufaa anayesikiliza kesi hiyo alifunga ushahidi na utetezi wa pande zote mbili (upande wa mashitaka na utetezi), baada ya waliopangwa kutoa ushahidi kumaliza jana.

Jaji Massati alianza kusikiliza kesi hiyo akiwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Ana kibali cha Jaji Mkuu kuendelea kusikiliza kesi hiyo.
Waliotoa ushahidi jana ni Juma Mohamed Mussa ambaye alitoa ushahidi dhidi ya mshitakiwa wa pili, Christopher Bageni na Moris Nyangerera aliyekuwa akitoa ushahidi dhidi ya Festus Chenge.

Jaji Massati aliwauliza mawakili wa upande wa utetezi iwapo kuna mmoja wao anataka kuleta shahidi mwingine, lakini kila wakili aliyesimama alisema hana mpango wa kuleta shahidi.

Baada ya kuwahoji mawakili hao, Jaji Massati alisema ushahidi umefungwa rasmi na leo mawakili wa upande wa utetezi watatoa hoja za mwisho kuthibitisha kuwa wateja wao hawana kesi ya kujibu.

Upande wa mashitaka nao utasimama kutoa hoja ya mwisho kuwa kwa ushahidi walioufikisha mahakamani hapo dhidi ya washitakiwa hao kwa pamoja wana kesi ya kujibu kwenye kesi hiyo ya mauaji.

Wakati huo huo, shahidi aliyeitwa kumtetea Bageni alijikuta akichanganya ushahidi wake na ule uliotolewa na mwenyewe wakati akijitetea.

Akihojiwa na wakili wa upande wa mashitaka, Jasson Kaishozi, Mussa alidai kuwa siku ya tarehe 14/1/2006 ambayo ndiyo siku walipouawa wafanyabiashara hao, bosi wake Bageni alikuwa ofisini tangu asubuhi wakati Bageni kwenye utetezi wake wa Februari mwaka huu alidai kuwa siku hiyo hakuwa ofisini.

Wakati alipokuwa akijitetea, Bageni alidai kuwa siku hiyo alikuwa shambani kwake Pugu na kwamba hata redio call yake yenye namba 122 ilikuwa haipatikani kwa kuwa huko alikokuwa hakukuwa na mawasiliano.

Vilevile, shahidi huyo wa Bageni alidai kuwa haamini kama kweli watuhumiwa wa ujambazi wamekufa kwani si kawaida ya polisi kukamata wahalifu na kuwaua.

Alidai kuwa hata yeye alistaajabu kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa watuhumiwa wa ujambazi waliokamatwa Sinza Palestina wameuawa katika mapambano ya kurushiana risasi na polisi.

Alidai kuwa waliwakamata watuhumiwa hao wanne wakiwa hai na hakukuwa na purukushani yoyote kwani baada ya kuwakamata waliwafunga pingu na kuwapandisha katika gari lao.

Sehemu ya mahojiano ya wakili wa upande wa mashitaka, Jasson Kaishozi na Morisi Nyangerera yalikuwa hivi:

Kaishozi: Mlipotoka Sinza baada ya kuwakamata watuhumiwa mkawahoji na kuwapekua wewe ulienda wapi?

Moris: Kituo cha Polisi Urafiki.
Kaishozi: Gari la wale watuhumiwa nani aliliendesha?

Moris: Mimi ndiye nilikuwa naliendesha na katika gari hilo tulikuwa mimi na Festus Chenge, ambaye alinishikia silaha yangu aina ya SMG.

Kaishozi: Wale watuhumiwa wanne mliowakamata walipelekwa wapi?

Moris: Kituo cha Polisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kaishozi: Hivi ni kawaida katika utendaji wa Jeshi mnapokamata wahalifu vielelezo vinaenda kwingine na watuhumiwa wanaenda kituo kingine?

Moris: Si jambo la ajabu labda ningeambiwa nilipeleka nyumbani kwangu huenda hapo ningeshangaa, lakini kupeleka kituo cha polisi si kitu cha ajabu.

Kaishozi: Sasa hebu niambie, ulipofika kituo cha Urafiki ulifanya nini pale?

Moris: Nilipaki ile gari ya watuhumiwa na nikamkabidhi OCS wa pale kwa maandishi.

Kaishozi: Baada ya kukabidhi gari mlienda wapi?
Moris: Mimi na Festus tulipanda daladala hadi Ubungo tukachukua gari tena hadi njia panda Chuo Kikuu kule Survey kuendelea na doria kama kawaida.

Kaishozi: Hebu ieleze mahakama hii habari za kuitwa kupongezwa na Zombe ulizipata wapi?

Moris: Nilikuwa nyumbani napumzika baada ya kutoka doria ndipo nilipoambiwa na Station Sajini James kuwa tunaitwa kwa Zombe. Wakati ule alikuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Dar es Salaam.

Kaishozi: Ehe baada ya kupata taarifa hizo ulifanya nini?

Moris: Nilivaa magwanda yangu na kwenda kazini.
Kaishozi: Je, waliwaambia mnakwenda kwa Zombe kufanya nini?

Moris: Hapana navyojua walitueleza kuwa tunaitwa kwa Kamanda tu.

Kaishozi: Baada ya kufika ofisini kwa Kamanda Zombe nini kiliendelea?

Moris: Alitushika mkono akatupongeza na kuamuru tupandishwe vyeo kwa kazi nzuri ya kukamata majambazi.

Kaishozi: Unakumbuka mlikuwa wangapi mliopewa mkono wa pongezi na Zombe?

Moris: Ndiyo, nakumbuka nilikuwa mimi, Mabula, Chonza, Michael na Noel.

Kaishozi: Kwa hiyo mkapewa pongezi.
Moris: Ndiyo, pongezi ya kukamata majambazi na mkuu wa kituo chetu cha kazi (OCS) aliamriwa kuandika mapendekezo sisi tupandishwe vyeo.

Kaishozi: Wakati mnapewa pongezi wale mliowakamata Sinza walikuwepo?

Moris: Hapana.
Kaishozi: Je, mlielezwa kuwa wako wapi?
Moris: Hilo ni suala la viongozi wao sio mimi na wala sina uwezo wa kuwahoji sisi kwenye jeshi tuna nidhamu ya hali ya juu. Mtu akikuzidi hata ngazi moja unamheshimu sana.

Kaishozi: Wale mliowakamata ulisema mliwakamatia wapi vile?

Moris: Sinza Palestine kwa mama mmoja anaitwa Benadetha Ngonyani.

Kaishozi: Katika kuwakamata kulikuwa na purukushani za aina yoyote ile?

Moris: Hakukuwa na vurugu maana tuliwakamata na kuwafunga pingu.

Kaishozi: Ina maana mliwakamata wakiwa wazima?
Moris: Ndiyo, walikuwa wazima kabisa.

Kaishozi: Mkuu wa kituo cha Urafiki, Ahmed Makelle aliamuru hao watuhumiwa wapelekwe wapi?
Moris: Kituo cha Urafiki.

Kaishozi: Hivi ulisema baada ya kuwapekua mliwakuta na nini?

Moris: Festus (mshitakiwa wa 13) alikuta bastola ya Chinese.

Kaishozi: Nawewe si ulishiriki kuwakamata wale watuhumiwa?

Moris: Ndiyo.
Kaishozi: Kwa hiyo taarifa za kwamba wale watuhumiwa walipambana na polisi Ukuta wa Posta ni za uongo?
Moris: Ni za uongo.

Kaishozi: Ulipogundua kwamba taarifa hizo ni za uongo uliwahi kutoa taarifa popote?

Moris: Hapana
Kaishozi: Haya ieleze mahakama hii tukufu, uliwahi kutoa maelezo yako kwenye Tume yoyote ile?

Moris: Ndiyo nilitoa maelezo kwa Tume ya Jaji Mussa Kipenka, ile ya Polisi na ya ACP, Sidney Mkumbi.

Kaishozi anamwonyesha maelezo ambayo inasadikika kuwa Moris aliyatoa kwenye Tume ya Jaji Kipenda kuhusu mauaji ya wafanyabiashara hao.

Moris alipoambiwa ayasome alianza kuyakana kwamba si maelezo yake.

\"Nimesema uyasome hayo maelezo yote sijakwambia kama ni maelezo yako,\" alisema Kaishozi na ndipo Moris alianza kuyasoma huku akisisitiza kuwa si yake.

``Mtukufu Jaji nayasoma haya maelezo, lakini si yangu.``
Maelezo hayo ya Moris kwa Tume ya Jaji Kipenka yalikuwa yanasema kwamba wafanyabiashara wale waliuawa katika mapambano ya kurushiana risasi na polisi kwenye Ukuta wa Posta tofauti na maelezo aliyotoa jana kuwa hakukuwa na mapambano yoyote.

Hata hivyo, baada ya kumaliza kuyasoma, Moris alimweleza Kaishozi kuwa maelezo hayo yanafanana fanana na yale aliyoyatoa kwenye Tume ya Kipenka, lakini si ya kwake.

Mahojiano kati ya wakili wa upande wa mashitaka Angaza Mwipopo na shahidi wa mshitakiwa wa pili Christopher Bageni, Juma Mussa, yalikuwa hivi:
Mwipopo: Mussa umeapa hapa mahakamani kwamba utasema ukweli si ndiyo?

Mussa: Ndiyo.
Mwipopo: Wito wa kuja hapa uliupata lini?
Mussa: Nimepigiwa simu leo asubuhi.

Mwipopo: Ni nani alikupigia simu?
Mussa: Wakili Ishengoma nikiwa msibani.
Mwipopo: Umerudi lini kutoka msibani?
Mussa: Juzi usiku.

Mwipopo: Juzi usiku ulifika saa ngapi kutoka huko msibani Singida.
Mussa: Saa 1.30 usiku.

Mwipopo: Kwa hiyo ina maana jana (juzi)
ulishinda nyumbani tu.

Mussa: Ndiyo.
Mwipopo: Ruhusa uliyoomba ya kwenda msibani imeisha bado?

Mussa: Imeisha, lakini nimeomba niongezewe.
Mwipopo: Kutoka Singida hadi hapa ulitumia usafiri gani?

Mussa: Lori.
Mwipopo: Ulitoka Singida na Lori hadi Dar?
Mussa: Ndiyo.

Mwipopo: Sisi tuliambiwa kuwa ulipanda basi lilipoharibika ndipo ukapanda lori kweli si kweli?
Mussa: Si kweli.

Mwipopo: Ulipoitwa mahakamani kuja kutoa ushahidi uliwaambia viongozi wako?

Mussa: Niko likizo hivyo niko huru.
Mwipopo: Polisi uko kitengo gani?
Mussa: Dereva.

Mwipopo: Dereva sio kitengo ina maana wewe askari hujui maana ya kitengo, namaanisha Trafik, CID, nk.
Mussa: CID.

Alipohojiwa na wakili wa Zombe, Jerome Msemwa, Moris ndipo alipodai kuwa bosi wake, Bageni, siku ya tarehe 14/1/2006 alikuwa kazini kama kawaida.

Jumatatu wiki hii Zombe kupitia wakili wake, Jerome Msemwa, aliiomba Mahakama hiyo impe nafasi ya kujitetea upya, lakini ombi lake hilo liligonga mwamba.

Awali, Zombe alitaka kutoa tena ushahidi wa namna ambavyo barua anazodai ziliandikwa na washitakiwa wenzake na zikatoka gerezani kinyume cha utaratibu kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP).

Zombe alidai kuwa barua hizo zilizopelekwa kwa DPP na washitakiwa wenzake, ndizo zilisababisha afunguliwe mashitaka hayo yanayomkabili.

Akitoa uamuzi kuhusu ombi hilo la Zombe, Jaji Salum Massati alisema hakuna sababu za msingi ambazo zinaweza kuishawishi mahakama kumruhusu Zombe kusimama kujitetea kwa mara ya pili.

Mbali na Zombe washitakiwa wengine ni, Christopher Bageni, Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Chonza, Abeneth Saro, Rajabu Hamis na Festus Chenge.

Katika kesi hiyo, washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka manne ya mauaji.

Wanadaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, Ephraimu Chigumbi, Mathias Lukombe na dereva teksi Juma Ndugu.

Kesi hiyo ilianza kuunguruma Mahakama Kuu Machi mwaka jana.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.