08 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Simba `yaitunishia misuli` TFF
 
2009-05-08 12:09:54
By Jimmy Charles

Uongozi wa klabu ya soka ya Simba umeeleza kwa sasa una uwezo wa kumuajiri Katibu Mkuu pekee yake kinyume na taratibu mpya za Shirikisho la soka nchini (TFF).

TFF imetoa maelekezo kwa klabu zote za Ligi Kuu kuajiri watu watatu, Katibu Mkuu, Mhasibu na msemaji wa klabu ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA).

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda, alisema kuwa klabu ya Simba haina uwezo wa kifedha na udhamini unaotolewa na kampuni ya bia nchini (TBL), ni mdogo hivyo kukidhi kulipa mishahara ya watu wote hao.

Kaduguda, alisema kuwa si kitu rahisi kuwalipa watendaji hao kutokana na kuhitaji mishahara minono, kitu ambacho ni kigumu kwa klabu yao.

Alisema kuwa wanatamani kutekeleza matakwa yote ya TFF na FIFA lakini hawana jinsi kwani hata kibinadamu suala hilo liko wazi na haliwezekani kwa klabu yao ya Simba.

Kaduguda, aliongeza kuwa fedha wanazopewa na mdhamini hazitoshi kutekeleza maagizo ya TFF, ambapo hata linapokuja suala la maandalizi ya timu pamoja na mishahara ya wachezaji bado fedha hiyo haitoshi kukidhi mahitaji yote.

Alisema kuwa tayari mchakato wa kutafuta katibu wa kuajiriwa umeanza, ambapo juzi aliiandikia kamati ya usaili kuwataka kuwasilisha kwa Kamati ya Utendaji majina ya watu waliojitokeza kuomba nafasi hiyo.

Akizungumzia usajili, Kaduguda, alisema kuwa wanajipanga kuanza mchakato huo mapema, ambapo fedha zitakazotolewa na mdhamini ambazo ni Sh. milioni 15, wataziweka kwenye akaunti maalum ambayo itahusika na masuala ya usajili.

Alisema tayari wameunda kamati ya watu 10, ambayo itasimamia masuala ya usajili, ambapo itaongozwa na Kassim Dewji, atakayesaidiwa na Evance Aveva huku wajumbe wakiwa ni Hans Pope, Geofrey Nyange, Salim Abdalah, Malamu Ng\'ambi, Idd Senkondo, Harisson Mutembei, Issa Batenga na Crescentius Magori.

Wakati huo huo, uongozi wa Simba, `umeufyata mkia` kwa Shirikisho la soka nchini (TFF), baada ya kufuta msimamo wake wa kugomea wachezaji wake kujiunga na timu za mikoa yao inayotarajia kushiriki kwenye michuano ya kuwania kombe la Taifa linalotarajia kuanza keshokutwa.

Kaduguda alidai wamebadili maamuzi yao ya awali na kuwaruhusu wachezaji wao kujiunga na timu zao za mikoa.

Alisema kuwa wameamua kubadili msimamo wao kutokana na kuogopa kuzua mzozo usio na maana, ambao unaweza kusababisha baadhi ya viongozi wao kufungiwa.

  • SOURCE: Nipashe
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.