08 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Lini Watanzania watafaidi rasilimali zao?
 
2009-05-08 13:34:22
Na Meshack Kitunzi

Ni muda mrefu sasa Tanzania imekuwa ikishuhudia mfumuko wa vyanzo vya rasilimali nyingi hasa madini. Historia hiyo ni ndefu kwani imeanza tangu mwaka 1998, kipindi ambacho kulijitokeza utititiri wa machimbo mapya ambayo yaliendana sambamba na uzalishaji uliosababisha ukuaji wa haraka wa sekta ya madini pamoja na uwekezaji nchini.

Kukua kwa sekta hiyo kunafanya madini yachukue karibu nusu ya malighafi ambazo Tanzania inasafirisha na kuuza nje.

Mfano, tafiti mbalimba;i zinaonyesha kuwepo kwa uzalishaji wa tani mbili za dhahabu mnamo 1998 tofauti na 2005, ambapo takwimu zinaonesha vilevile kuwepo kwa zaidi ya tani 50 za aina hiyo ya madini nchini.

Matokeo ya uzalishaji huo yanaiweka Tanzania katika nafasi ya tatu barani Afrika kwa kuzalisha dhahabu baada ya Afrika Kusini na Ghana kuchukua nafasi ya kwanza na pili.

Hata hivyo kuwepo kwa faida kubwa na soko linalokuwa haraka katika rasilimali hiyo bado faida hizo zimeendelea kuonekana katika karatasi na takwimu tu.

Hali hiyo inatokana na kuendelea kuwepo kwa viashiria vya maisha duni yaliyomzingira Mtanzania wa kawaida hasa yule aishiye maeneo ya vijijini.

Aidha sababu inayotajwa na wachambuzi wengi wa sera na masuala ya madini ni kuwepo kwa sheria za kodi ambazo ni dhaifu.

Pamoja na ukweli kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa madini , inahesabika kwenye orodha ya nchi 10 duniani zenye hali mbaya na hivyo kuitwa masikini wa kutupwa duniani.

Ikiwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 39 wenye wastani wa kipato cha sh 399,873 sawa na dola 307 kwa mwaka huku umri wa kuishi ukiwa miaka 48 na watu zaidi ya 400 wanaokufa kwa Ukimwi kila mwaka.

Matukio haya yote yanafanya nchi yetu ikabiliwe na changamoto kubwa hasa zenye kuhitaji utatuzi wenye kuambatana na maamuzi mazito yasiyojali nani ni nani ilimradi kila mtu anashiriki katika kuzikabili changamoto hizo.

Hali hiyo inaibua maswali kadhaa kama vile iwapo ni muhimu kuwepo kwa machimbo mengi ya dhahabu wakati faida kubwa haionekani?

Hata hivyo inaelezwa kuwa nchi yetu inaweza kuendelea kuteseka na hali hiyo ya kutofaidi madini yake iwapo marekebisho makubwa katika sekta hiyo hayatafanywa na hivyo kumpa mwekezaji wa ndani nafasi ya kuendesha migodi hiyo jambo ambalo litasaidia uchumi kukua.

Hali hiyo imetokana na nchi yetu kubadili uchumi wake kuwa wa kiliberali miaka iliyopita ikiwa ni shinikizo la Benki ya Dunia nyuma ya pazia la marekebisho ya kiuchumi ya mnamo 1986. Ingawa kama zingefuatwa inavyopasa tungefaidika.

Aidha kampuni za uchimbaji zinalipa asilimia tano tu ya kodi ya uingizaji vipuri na mitambo, jambo ambalo ni tofauti na wawekezaji katika sekta nyingine ambao hulazimika kulipa asilimia 10 mara watakapo kufanya hivyo.

Kwa mfano, tafiti zinaonyesha kuwa mnamo 2004 hadi mwaka juzi, kampuni sita za uchimbaji madini ziliripotiwa kuingiza nchini mafuta kwa ajili ya mitambo yao lita milioni 178 kitendo ambacho kilifanya kuikosesha serikali mapato zaidi ya bilioni 62.8 sawa na Dola milioni 60.

Bado serikali vilevile imeshindwa kuweka sheria nzuri za kuwabana wawekezaji wa madini katika kuajiri, jambo ambalo ni tofauti na sekta nyingine zisizokuwa za madini ambazo zimewekewa kiwango.

Benki ya Dunia haiwezi kukwepa lawama hizi kwani mwaka 1989 ilitoa maelekezo yaliyoitaka Tanzania kulegeza masharti kwa uwekezaji toka nje ikiwa ni sehemu ya kuvutia mitaji ya nje.

Itakumbukwa kuwa 1994, ulianzishwa mradi chini ya benki ya dunia ulioegemea zaidi kutoa msaada wa kiufundi katika sekta ya madini nchini.

Ni kutokana na hilo sera ya madini nchini ikatungwa mwaka 1997 ambayo inasisitiza zaidi kuwepo kwa ushirikishwaji wa karibu wa kampuni binafsi katika sekta hiyo.

Mmoja wa wanaharakati na watetezi wa mazingira hapa nchini ambaye pia ni mwanasheria, Tundu Lissu, anaishangaa serikali kutokana na kitendo chake cha kuendelea `kuwabeba` wageni wanaokuja kuwekeza katika sekta hiyo huku ikiwafukuza wakazi wa eneo yanapogundulika madini.

Tangu kuundwa kwa sera hizo zilizogusia zaidi katika eneo la sheria, tozo, kodi na suala la mitaji ambazo kwa pamoja zililegeza na kupunguza viwango vya kodi katika eneo hilo sambamba na uhamishaji wa faida yote itokanayo na uchimbaji madini toka ndani.

Ushahidi ni mwingi kuwa bado nchi yetu ina ombwe la utawala ambao ungeweza kutetea vizuri rasilimali za nchi na hivyo kukabiliana na umasikini unaotukabili.

Meshack Kitunzi ni mwandishi wa habari wa kujitegemea simu: 0716492992

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.