08 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Polisi walioua kuranda mitaani ni fedheha
 
2009-05-08 13:42:19
Na Mhariri

Ipo mizigo miwili mikubwa juu ya mabega ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema. Hii ni askari wake watatu wanaotuhumiwa kuua raia watatu, mkoani Arusha na jijini Dar es Salaam.

Tayari kamati mbili tofauti, yaani ile iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore Shirima na ile iliyoundwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, zilikwisha kutoa ripoti juu ya mauaji haya na kueleza wazi kwamba waliouawa hawakuwa majambazi.

Mjini Arusha waliuawa vijana wawili Machi mosi mwaka huu, Goodluck Olais Motika (22) na Eward Joseph Mtui (36), wakati jijini Dar es Salaam eneo la Kimara Stopover, kijana Lazaro Mwapi (34) aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi Aprili. Kote huko polisi walizusha kwamba waliouawa walikuwa ni majambazi.

Matukio haya yanafanana na lile la Januari 14, 2006 lilitokea jijini Dar es Salaam ambalo wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, waliuawa na polisi na kusingiziwa kwamba walikuwa ni majambazi.

Tunajua kwamba kwa sasa ipo kesi ya mauaji Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam ikiwakabili polisi tisa, akiwamo aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam pia akiwa ni Mkuu wa Upelelezi wa mkoa huo, Abdallah Zombe.

Kesi hii bado inaendelea na hatuna sababu ya kuingia uhuru wa mahakama kwa kuwa tunaamini kwamba haki itatendeka.

Lakini kilio chetu leo ni kuona jinsi suala zima la polisi wanaotuhumiwa kuua vijana wawili mjini Arusha na mmoja jijini Dar es Slaam, linavyoendeshwa.

Taarifa ambazo zimezagaa mitaani na ambazo hatuna sababu za kuzipuuza kwa sababu zinaeleza undani wa matukio haya mawili, polisi waliohusika na mauji haya bado wako kazini, wanaendelea na kazi kana kwamba hakuna kilichotokea.

Kila mmoja kwa nafasi yake, yaani Kandoro ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, na mwenzake wa Arusha, walipotangaza ripoti za kamati zao, walisema wazi kwamba imethibitika vijana waliouawa hawakuwa majambazi na kwamba taarifa zimepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya taratibu zaidi za kisheria.

Tunajiuliza kwamba hadi sasa umma haujui kinachoendelea juu ya hatua hizi za kisheria wananchi wanataka kujua ni lini askari polisi waliohusika katika kadhia hii watafikishwa mahakamani ili walau imani ya wananchi kwa chombo hiki chenye dhima ya kulinda maisha na mali zao irejee?

Swali hili tunaliuliza si kwa sababu polisi hawa wakifikishwa mahakamani uhai wa waliouawa utarejeshwa, ila wazazi na marehemu wote walau wataona kwamba kweli nchi hii inaendeleshwa kwa utawala wa sheria na si kwa matakwa na hisia za watendaji ndani ya serikali hasa polisi wanaotumia sihala za kuwalinda raia kuwaua wananchi wasio na hatia.

Tunatambua kwamba zipo taratibu za kufuata kabla ya kumfungulia mtu mashitaka mahakamani na hasa inapokuwa ni ya jinai, pamoja na kutambua hatua hizo, lakini tunahisi kwamba kasi si nzuri katika kutekeleza hayo la muhimu zaidi ni kwamba hatuioni mantiki ya watuhumiwa wa mauaji kuendekea na kazi ya upolisi wakati suala lao likiwa katika mkondo wa sheria. Hawa wakae kando wasubiri hatima yao.

Ni utaratibu wa kisheria kwamba mtu anayetuhumiwa kwa kesi kubwa kama mauaji hukaa kando wakati suala lake likishughulikiwa.

Ndiyo maana tunasema IGP Mwema ana mzigo begani mwake, tunadhani ni vema polisi hawa wakawekwa pembeni wakati taratibu nyingine za kisheria zikisubiriwa kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.