08 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

`Bodaboda` yaua na kujeruhi wanafunzi
 
2009-05-08 13:48:44
Na Wilbroad Tungaraza

Wanafunzi wawili waliokuwa wanasoma katika Shule ya Sekondari Ikoma wilayani hapa mkoa wa Mara wamepatwa na ajali mbaya iliyosababisha mmoja kufariki dunia na mwingine kujeruhiwa kichwani baada ya kugongwa na pikipiki maarufu kama Bodaboda wakiwa kwenye baiskeli.

Mwanafunzi aliyepoteza maisha katika ajali hiyo ni Daud Maguye (17) ambaye alipasuka kichwa na kuvunjika mkono na shingo wakati aliyejeruhiwa ni Alex Range (18) ambaye alipata majeruhi ya kichwani na kupoteza fahamu wote wakazi wa Robanda.

Akizungumza na Nipashe katika Hospitali Teule ya Nyerere DDH, Mganga wa zamu David Nyamokwe, alisema majeruhi alikuwa anaendelea vizuri licha ya kulalamika kichwa na kifua.

Mtendaji wa Kijiji cha Ikoma Robanda ambako wanafunzi hao wanatokea, Joseph Nkiri, alisema kwamba wanafunzi hao wanaosoma Kidato cha pili Mkondo B, walikumbwa na ajali hiyo katika kijiji cha Bwitengi juzi wakiwa wamebebana kwenye baiskeli.

Nkiri alisema kwamba waligongwa na pikipiki hiyo wakiwa wanarejea nyumbani kwao kijiji cha Ikoma Robanda Km 30 baada ya kufukuzwa na mkuu wa shule yao kwa kukosa mchango wa shilingi 5,000.

Watu walioshudia tukio hilo walisema kwamba marehemu alikuwa amembeba mwenzake katika baiskeli hiyo kabla ya kukumbana na Bodaboda iliyodaiwa kwenda kwa kasi na kuwagonga na mwendeshaji pikipiki kukimbia.

Wakati huo huo polisi inaendelea kumsaka mwendesha pikipiki aliyetoroka mara baada ya kumgonga muendesha baiskeli.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.