08 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

NCCR-Mageuzi Iringa wampongeza Mengi
 
2009-05-08 13:49:16
Na Mwandishi Wetu

Chama cha NCCR-Mageuzi Manispaa ya Iringa, kimempongeza Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kwa kutaja hadharani majina ya watu wanaojihusisha na ufisadi mkubwa na kuwapa jina la `mafisadi papa`.

Mwenyekiti wa chama hicho Manispaa ya Iringa, Fulgence Malangalila, katika taarifa yake ya pongezi aliyoituma kwa gazeti hili jana kwa niaba ya chama chake, alisema Mengi ameonyesha ujasiri wa hali ya juu kuwataja hadharani mafisadi wakubwa, kwani wengi wameshindwa kufanya hivyo na kubaki kulalamika chini kwa chini, kutokana na hulka ya Watanzania kuwaogopa matajiri na watu wenye madaraka.

``Kitendo cha ujasiri cha kuwataja majina `mafisadi papa` wa Tanzania kilichofanywa na Mtanzania huyo shupavu, ni kitendo ambacho Watanzania walio wengi wamekishangilia,`` alisema.

Alisema inasikitisha kuona baadhi ya watu wakijitokeza kupinga hatua ya Mengi kuwataja mafisadi hao badala ya kumuunga mkono, kwani ufisadi umechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Hata hivyo, alisema pamoja na watu hao kujaribu kudhoofisha vita dhidi ya ufisadi, lakini inatia moyo Watanzania wengi wanauchukia ufisadi na kumuunga mkono mtu yoyote anayejitokeza kuongoza mapambano hayo.

``Watanzania walio wengi wanaomba watu aina ya Mengi wajitokeze kutaja majina ya `mafisadi papa` ambao wanashika nyadhifa za serikali, mawaziri na wabunge, kwani mawakala wa kutengeneza na kueneza chuki dhidi ya Mengi wamekuwa mstari wa mbele kuharibu sifa yake bila ya sababu za msingi,`` alisema.

Amemsifia Mengi, kusadia jamii na makampuni yake kutoa ajira nyingi, tofauti na mafisadi ambao wamekuwa wakiliibia taifa na kuzidisha umasikini kwa Watanzania wengi.

``Watanzania wanawauliza hawa vinara wa chuki kwamba kuna Mtanzania gani ambaye amempita Mengi kutoa misaada kwa vikundi vya vijana wasio na ajira zaidi ya 500,000 kwa mkupuo.

Mengi sasa anajenga hospitali ya kutibu Watanzania wenye matatizo ya moyo kwa gharama kubwa baada ya kushuhudia vifo vya wagonjwa wengi wanaopelekwa India kwa matibabu,`` alisema Malangalila.

Alimtaka Rais Jakaya Kikwete, kumzawadia Mengi nishani ya pili baada ya ile ya Martin Luther King, aliyotunukiwa na Ubalozi wa Marekani nchini, badala ya kusikiliza watu wanaojaribu kutafuta sifa za kisiasa kwa ajili ya kuganga njaa.

Pia alikemea kauli ya Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, kuwa suala la Mengi na mafisadi limefungwa na kuiita kuwa siyo sahihi.

``Hana mamlaka ya kuwakataza Watanzania wasiendelee kulijadili suala hili kwani hakulianzisha yeye aliache kama lilivyo,`` alisema Malangalila.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.