08 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kibaka aduwaza walinzi Ikulu
 
2009-05-08 13:51:35
Na Jacqueline Mosha

Mfanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam, Ally Nasoro (41) amefikishwa mahakamani kujibu shitaka la kuingia Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete na kuiba ua moja lenye thamani ya Sh. 5,000, mali ya Ikulu hiyo.

Mshitakiwa huyo alifikishwa mbele ya Hakimu Mwajuma Diwani wa Mahakama ya Mwanzo Kariakoo jijini Dar es Salaam jana, na kusomewa shitaka hilo.

Akisoma hati ya mashitaka, karani wa mahakama hiyo, Caphren Maduhu, alidai mbele ya hakimu Diwani kuwa mshtakiwa alifanya kitendo hicho Mei 2 mwaka huu.

Mahojiano mahakamani hapo yalikuwa kama ifuatavyo:
Karani: Kesi hii ni ya wizi na imefunguliwa na mlalamikaji ambaye ni askari mwenye namba E 4716 Koplo Mnyaga.

Mshitakiwa katika shitaka hili ni Ally Nasoro, anaishi eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam na anakabiliwa na kosa wizi alilofanya Mei 2, mwaka huu, saa 4:24 usiku huko Ikulu ya Rais.

Hakimu: Mshitakiwa umesikia mashitaka ya kosa lako, unajibu nini?

Mshitakiwa: Mimi nilikuwa napima uwezo wa akili wa walinzi waliowekwa Ikulu ili kumlinda Rais wa nchi, maana isije ikawa wako wako tu kumbe hawana hata uwezo wa kumlinda.

Hakimu: Ile ni sehemu ya heshima na inalindwa iweje wewe upate wazo la kutaka kuingia ndani, ulikuwa na nia gani?

Mshitakiwa: Nililichokigundua siku hiyo ni kwamba kumbe naweza kuingia Ikulu kiulaini bila hata ya kuguswa na mtu.

Kwanza nilipofika pale getini nilitaka kufahamu kama naweza kufanikiwa kuingia, hivyo, nilisimama kwa saa nne nje ya geti bila hata kuulizwa chochote na walinzi.

Baadaye nilifanikiwa kupata mwanya wa kuingia ndani na kweli niliingia kiulaini bila hata `shobo.

Hakimu: Ilikuwaje mpaka ukaiba hilo ua?
Mshitakiwa: Nilipolichukua lile ua na kulibeba ndipo walinzi waliniona na baada ya kuniona walinzi hao walibaki wakitetemeka huku mimi nikiwa nimeshikilia ua na ndipo waliponikamata na kunichukulia hatua.

Kama naweza kuchukua ua si ningeweza hata kuingia ndani kwa Rais kiulaini? Yaani walinzi wamelala pale. Hawako makini kama nilivyodhani.

Hakimu: Unajibu nini kuhusu shitaka la wizi huo?
Mshitakiwa: Si kweli, sijaiba ua.

Hakimu Diwani aliahirisha kesi hiyo mpaka itakapotajwa tena mahakamani hapo Mei 11 mwaka huu. Mshitakiwa alipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ambayo ni kuwa na wadhamini wawili.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.