08 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mawakili wa Zombe walia na Koplo Lema
 
2009-05-08 13:58:56
Na Hellen Mwango na Joseph Mwendapole

Mawakili wa utetezi kwenye kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini na dereva teksi mmoja, inayomkabili aliyekuwa Kaimu Kamanda na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake, wame onekana kuuhofia ushahidi uliotolewa na aliyekuwa mshitakiwa wa 11, marehemu Koplo Rashid Lema na wameisihi Mahakama Kuu isiutumie katika kufikia hukumu.

Kila wakili wa utetezi aliyesimama jana aliiomba mahakama isiutumie ushahidi huo wakidai kuwa mwenyewe hakusimama mahakamani hapo kuthibitisha alichoandika kwenye maelezo yake kwa Tume ya Jaji Mussa Kipenka.

Wa kwanza kuomba ushahidi huo usitumike mahakamani hapo ni wakili wa Zombe, Jerome Msemwa akifuatiwa na wakili Gaudionus Ishengoma anayemtetea Christopher Bageni ambaye ni mshitakiwa wa pili pamoja na Majura Magafu anayewatetea washitakiwa wa 3,5,7,9 na 10.

Lema ndiye aliyefichua siri ya mauaji hayo kwa kudai kuwa waliouwawa hawakupambana na polisi bali walichukuliwa wakiwa hai kutoka Sinza jijini Dar es Salaam na kupelekwa msitu wa Pande uliko Mbezi Louis ambako walipigwa risasi mmoja baada ya mwingine.

Magafu alimwomba Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Salum Massati kutupilia mbali ushahidi wa Koplo Lema kwani hakuna ushahidi mahakamani pale kwamba mauaji yalifanyika msitu wa Pande.

``Kama Lema kafa basi kaenda na maovu yake. Binadamu anarithi mali si maovu na kama kuna mali basi itarithi familia yake na si hawa washitakiwa,`` alidai Magafu.

Aliendelea kudai kuwa mahakama haitakiwi kukuzingatia ushahidi ambao mhusika hakusimama kizimbani na kuuelezea kama ilivyotokea kwa Koplo Lema.

Magafu alidai kuwa hilo linaweza kufanyika tu endapo itabainika kuwa upande mmoja kwenye kesi umefanya hujuma ili asihojiwe.

``Mtukufu Jaji kwa kuwa upande wa utetezi haujasababisha Lema asihojiwe, basi naiomba mahakama yako tukufu ushahidi huo utupwe ili wateja wetu wasihukumiwe kwa kosa ambalo si lao,`` alidai.

Alidai kuwa ushahidi wa Lema hauwezi kuisaidia mahakama kuthibitisha kuwa mauaji yale yalifanyika katika msitu wa Pande kama alivyodai Lema katika maelezo yake kabla hajafariki dunia.

Aliendelea kudai kuwa maelezo mengine yanayotaka kuonyesha kuwa mauaji yalifanyika msitu wa Pande na kwamba wateja wake ambao ni mshitakiwa wa 3,5 na 10 walikwenda kwenye msitu huo yalitolewa kama maelezo ya onyo ya mshitakiwa wa 12, Rajabu Bakari na hivyo akataka mahakama iyatupilie mbali.

Alidai kuwa hakuna ushahidi unaothibitisha bila shaka kuwa wateja wake walikwenda katika msitu huo ingawa wamekiri kuwa walihusika katika kuwakamata waliodaiwa kuwa majambazi.

Magafu alidai kuwa baada ya zoezi la kuwakamata waliodaiwa kuwa majambazi, mshitakiwa wa 3,5,9 na 10 waliendelea na maeneo yao ya doria.

Katika maelezo yake kwa Tume ya Kipenka, Lema alidai kuwa alikaa mafichoni, lakini aliamua kuibuka na kusema ukweli kwa sababu nafsi yake ilikuwa ikimsuta kutokana na mauaji yale.

Lema aliiambia Tume hiyo, kwamba wafanyabiashara hao walichukuliwa wakiwa hai na kupelekwa msitu wa Pande ambako waliuwawa mmoja baada ya mwingine wakiwa wamelazwa kifudifudi.

Lema alidai kuwa askari aliyekuwa akiwafyatulia risasi ni Koplo Saad, ambaye hadi leo anaendelea kutafutwa ili aunganishwe kwenye kesi hiyo.

Wakili Ishengoma anayemtetea mshitakiwa wa pili, Christopher Bageni, aliiomba mahakama itupilie mbali ushahidi uliotolewa na Koplo Lema kwa sababu zinazofanana na zile zilizotolewa na mawakili wengine.

Ishengoma alidai kuwa hakuna ushahidi wa uhakika kuwa mteja wake alikuwepo siku ya tukio la mauaji.
Alidai kuwa siku hiyo ya Jumamosi, Bageni hakuwa kazini na alikuwa shambani kwake Pugu.

Ishengoma alidai kuwa shahidi Juma Mussa aliyedai kuwa Bageni alikuwa kazini tarehe 14/1/2006 ni muongo.

Kwa upande wake, Magafu anayewatetea washitakiwa wa 3,5,7,9 na 10 alidai kuwa ushahidi unaojaribu kuwahusisha wateja wake na mauaji hayo si wa moja kwa moja na ni wa kuungaunga.

Alidai kuwa hakuna ubishi kuwa marehemu wote wanne walikamatwa wakiwa hai na hakukuwa na purukushani wala kurushiana risasi.

Magafu alidai kuwa maelezo hayo yanaungwa mkono na mashahidi walioshuhudia marehemu walipokuwa wakikamatwa kule Sinza Palestina.

Magafu alidai kuwa upande wa mashitaka umeleta mkanganyiko mkubwa kwenye kesi hiyo.

Alidai kuwa wapelelezi wa kesi hiyo hawakuwa makini na waadilifu, ndiyo sababu wamevuruga na kusababisha mkanganyiko.

Alidai kuwa jambo hilo inawezekana lilifanywa kwa makusudi au kwa uzembe na hivyo akasema: ``Hivyo (kutokana na mkanganyiko) hata haya mauaji haijulikani mpaka leo yalifanyika wapi,`` alidai.

Aidha, Magafu aliendelea kudai kuwa wakati upande wa mashitaka ukidai kuwa mauaji yalifanyika msitu wa Pande, baadhi ya mashahidi waliopelekwa mahakamani hapo na upande wa mashitaka walidai kuwa waliouwawa walikuwa wakipambana na askari katika Ukuta wa Posta.

Alidai kuwa hata shahidi wa 27 wa upande wa mashitaka ambaye ni ofisa wa juu katika Jeshi la Polisi alitoa ushahidi kuwa kulikuwa na mapambano.

Magafu alidai kuwa hata shahidi wa 22 ambaye ni askari alisema kulikuwa na mapambano ya kurushiana risasi.

``Afande Nikobai alikuja hapa akasema walikuta damu Ukuta wa Posta na waliokota mapande ya damu Ukuta wa Posta,`` alidai.

Alidai kuwa damu hiyo inadaiwa kuwa ilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, lakini majibu yake hadi leo hayajawasilishwa mahakamani hapo.

Mkanganyiko mwingine kwa mujibu wa Magafu ni wa mashahidi wa 30,31 na 36 wa upande wa mashitaka waliodai kuwa mauaji yalifanyika msitu wa Pande.

``Hakuna ubishi kwamba watu waliuwawa tena kwa risasi, lakini Mtukufu Jaji, hadi leo kuna swali tunajiuliza. Hao watu waliouwawa ni wapi na nani aliyewaua... Upande wa mashitaka wangekuwa makini haya yote yasingetokea,`` alidai.

Magafu alidai kuwa upande wa mashitaka unataka kuishawishi mahakama iamini kuwa washitakiwa walikula njama za mauaji ya watu wanne wakati ushahidi wa kuonyesha kuwa kulikuwa na njama haujawasilishwa mahakamani hapo hadi jana.

\"Hivi hawa washitakiwa walikaa vipi pamoja wakapanga njama za mauaji? Ni dhahiri ushahidi huo haupo na ndiyo sababu mahakama hii ikaamua kuwaachia huru mshitakiwa wa 4, 6 na 8.

Alidai kuwa endapo kungekuwa na njama za mauaji hata washitakiwa ambao waliachiwa huru wasingeachiwa.

Alidai kuwa upande wa mashitaka ulipaswa kuwasilisha ushahidi kuthibitisha kuwa mauaji yalifanyika kwa makusudi au kulikuwa na nia ya makusudi ya kusababisha mtu afe, jambo ambalo alidai wameshindwa kufanya.

Akitoa hoja za mwisho kuthibitisha kuwa mteja wake hana hatia, Wakili wa Zombe, Jerome Msemwa alidai kuwa hivi sasa wananchi wanamchukia mteja wake kutokana na vyombo vya habari kumhukumu kwa kumuandika vibaya.

Msemwa alidai kuwa vyomba vya habari vimekuwa vikiandika kuwa Zombe hachomoki lazima atanyongwa.

``Mtukufu Jaji, hata Yesu alihukumiwa na Pilato wakati hakuwa na kosa na watu wote wa Galilaya walimlilia wakisema ni mwana wa Mungu, lakini mwisho wake alifufuka na kudhihirisha kuwa ni mtu mwema kama Zombe. Naomba mahakama imuachie huru mteja wangu kwa sababu hahusiki na mauaji,`` alidai Msemwa.

Alidai kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kutoa ushahidi wa moja kwa moja kwamba Zombe amewaua wafanyabiashara wale.

Alidai hakuna shahidi aliyesema Zombe alishirikiana na wenzake kupanga mipango ya mauaji hayo na kwamba hata alipojitetea alieleza mahakama namna alivyopokea taarifa za matukio na mauaji yaliyotokea siku ya tukio hilo.

``Mtukufu Jaji, Zombe alipokea taarifa ya maandishi na barua ya tukio la mauaji hayo kwamba waliouawa walikuwa ni majambazi na ni utaratibu wa kawaida kwa Mkuu wa Polisi wa Mkoa kupokea taarifa kwa njia ya maandishi kutoka kwa makamanda wa upelelezi wa eneo lake la kazi,`` alidai.

Wakili huyo alidai kuwa washitakiwa kudai kuwa walipewa vikaratasi vya maelekezo ya namna ya tukio lilivyokuwa ilielezwa kwenye maelezo ya marehemu Rashidi Lema, lakini hakuna shahidi wa upande wa mashitaka aliyeunga mkono maelezo hayo dhidi ya Zombe.

Aidha, alidai pia hatua ya Zombe kwenda Kituo cha Polisi Urafiki ni sehemu ya majukumu yake ya kazi ambayo alitekeleza siku hiyo baada ya kupigiwa simu na Mkuu wa Kituo cha Polisi Urafiki kwamba kuna tatizo la fedha za kielelezo zimepotea.

Alidai kuwa Zombe alitoa amri zipatikane na kweli siku ya pili yake mteja wake alikabidhiwa, lakini upande wa mashitaka haujaziwasilisha mahakamani hapo.

Msemwa aliongeza kuwa tukio hilo limeongelewa na upande wa mashitaka na washitakiwa wa pili, Christopher Bageni na wa tatu Ahemed Makelle ambao wameieleza mahakama.

``Mtukufu Jaji kuwapongeza washitakiwa ni kawaida kwa Jeshi la Polisi kwa wanaofanya vizuri, na sio wazo binafsi la Zombe. Hizi ni taratibu za kiofisi,`` alidai.

Alidai kuwa mteja wake amelalamikia mahakama huhusu hatua ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) aliyestaafu Godfrey Shaidi, kumshitaki baada ya kufanya mawasiliano na washitakiwa wenzake wakiwa gerezani ambapo alizitumia kama kigezo cha kumfungulia mashitaka.

``Bila kuacha shaka, mteja wangu hakushiriki kupanga wala kufanya mauaji hayo na naiomba mahakama hii isimtie hatiani, imuachie huru,`` alidai Msemwa.

Naye wakili Denis Msafiri anayemtetea Rajabu Hamis alidai kuwa mteja wake alikuwa muungwana na kwamba alieleza jinsi ukweli na mtiririko mzima wa tukio hilo akiwa na kiongozi wake Bageni.

Upande wa mashitaka uliomba shauri hilo liendelee leo ili watoe hoja zao dhidi ya washitakiwa.

Hata hivyo, Jaji Massati alisema kesi hiyo haiwezi kuendelea leo kwani ilikuwa imepangwa isikilizwe hadi jana tu na itaendelea tu pale Jaji Mkuu wa Tanzania atakapotoa kibali.

Mbali na Zombe washitakiwa wengine ni Christopher Bageni, Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Chonza, Abeneth Saro, Rajabu Hamis na Festus Chenge.

Katika kesi hiyo, washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka manne ya mauaji, Januari 14, mwaka 2006 wanadaiwa kuwa waliwaua wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, Ephraimu Chigumbi, Mathias Lukombe na dereva teksi Juma Ndugu.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.