26 Apr 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kondic: Mvua ya magoli pale pale Villa
 
2009-04-26 14:05:43
By Mwandishi Wetu

Mabingwa wa soka Bara, timu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, leo inacheza na Villa Squad katika mchezo wa mwisho wa kufunga pazia la ligi hiyo unaofanyika kwenye uwanja wa Uhuru jijini.

Yanga iliyotwaa ubingwa mapema leo itacheza bila hofu huku wakitaka kuwaangamiza zaidi Villa ambao tayari wameshuka daraja ikitaka kujiwekea rekodi ya kuifunga timu hiyo kwa msimu mzima.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza Yanga \'iliinyeshea\' Villa mvua ya magoli 5-0.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Dusan Kondic alisema haidharau timu hiyo kwa kuwa tayari imeshuka daraja, na atahakikisha wachezaji wake wanacheza kwa bidii kama ilivyokuwa katika mechi nyingine zilizopita.

``Mechi zote ni sawa hakuna tofauti ya Villa au Mtibwa au timu nyingine yoyote hivyo sidhani kama tutaidharau,`` alisema Kondic.

Alisema wameendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo huo wa mwisho ambao ameahidi ushindi ili kujiongezea pointi zaidi ya walizonazo sasa 51 zilizotokana na ushindi wa mechi 16 na kutoka sare mechi tatu huku wakipoteza mechi mbili.

Yanga yenye udhamini wa kampuni ya bia nchini, TBL na kampuni ya simu za mkononi ya vodacom, ilifanya usajili wa nguvu, ambao umekuwa tishio kwa wachezaji wake kucheza kwa kujituma zaidi huku wakigombania namba kutokana na kuzidiana kiwango.

Lakini kwa Villa timu iliyofungwa magoli mengi zaidi katika ligi hiyo (49) na pia kufunga machache zaidi (17), nayo imeridhika kushuka kwao daraja lakini lawama zaidi wakiwatupia waamuzi kwa kuzipendelea baadhi ya timu.

Villa iliyopanda ikitokea wilaya ya Kinondoni imeshindwa kabisa kuhimili mikiki mikiki ya ligi hiyo na kujikuta ikiangukia pua baada ya kufungwa mechi mfululizo, licha ya kubadilisha kocha na kumtumia mzoefu Kenneth Mwaisabula.

  • SOURCE: Lete Raha
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.