26 Apr 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Simba kutinga CAF leo?
 
2009-04-26 14:13:35
By Mwandishi Wetu

Simba leo ndio siku ya mwisho kujua kama watashiriki Kombe la Shirikisho au la mwakani watakapomaliza mechi na timu iliyoshuka daraja ya Polisi Dodoma katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Simba, ambayo bado haijajihakikishia nafasi ya pili ya kucheza Kombe la Shirikisho Barani Afrika mwakani, imepania kushinda mchezo huo waliouita mgumu kutokana na Polisi kuwa tayari imeshuka lakini haitaki kufungwa.

Meneja wa timu hiyo ambayo mwaka 1993 ilitinga fainali ya Kombe la CAF, Innocent Njovu, alisema mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na wapinzani wao kutaka kuendeleza rekodi ya kuisumbua timu hiyo kongwe nchini. Timu hizo zilitoka sare ya magoli 2-2 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza jijini Dar es Salaam.

``Hawa Polisi sio kwamba watacheza kinazi kwa kuwa tayari wameshuka daraja, nina uhakika watacheza mchezo wao ule ule wa siku zote kwani nao ushindi au sare itakuwa ikiwaweka katika rekodi nzuri ya kuwa ilitusumbua msimu uliopita,`` alisema Njovu.

Lakini, alisema timu yake imejipanga vyema kumaliza mchezo huo na kushinda ili wapinzani wao wa karibu Mtibwa Sugar wasipate nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano hiyo ya pili kwa ukubwa Afrika kwa ngazi ya vilabu.

Njovu alisema kikosi chake hakina majeruhi na wachezaji wote ni wazima na tayari wapo mjini Dodoma tangu juzi Ijumaa tayari kwa mchezo huo muhimu.

Simba wanashika nafasi ya pili wakiwa wamejikusanyia pointi 37, huku Mtibwa waliopo katika nafasi ya tatu wana pointi 35 na endapo watashinda mchezo wa leo dhidi ya Polisi Morogoro, na Simba kupoteza watakuwa ndio wawakilishi wa pili baada ya Yanga watakaokuwa wakipeperusha bendera katika michuano ya mabingwa wa Afrika.

Simba iliboronga kwenye mzunguko wa kwanza ambapo ililazimika kuwatimua kwa nyakati tofauti makocha Jamhuri Kiwhelu na Krasmir Benziski na hatimaye kufundishwa kwa muda na kocha Talib Hilal, na sasa imemrudisha kocha wake wa zamani Patrick Phiri.

Kocha wa Polisi Dodoma, Juma Mwambusi alikaririwa akisema Simba wasitarajie mteremko leo licha ya kwamba timu yake imeshuka daraja.

Alisema timu yake itashuka dimbani kwa lengo la kuifunga Simba na kwamba itacheza soka la hali ya juu.

  • SOURCE: Lete Raha
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.