03 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Inspektah Haroun: Ni Gangwe tena!
 
2009-05-03 18:44:35
By Amour Hassan

Ni Gangwe Tena. Gangwe Iz Back, ndio kauli mbiu ya marejeo ya kundi lililotingisha kwenye miaka ya mwishoni mwa `90 hadi mwanzoni mwa 2000 la Gangwe Mobb.

Ni fursa nyingine tena ya kukumbushia mambo makubwa kama ya zama zile za `Ngangari` na `Mtoto wa Geti Kali`, amesema kinara wa kundi hilo.

Inspektah Haroun ameiambia Lete RAHA juzi Ijumaa kuwa baada ya takriban miaka sita tangu kuvunjika kwa kundi hilo, ``Gangwe Mobb Is Back.``

``Tunarejea tena, ni Gangwe tena,`` alisema rapa huyo.
``Tumejadili na Luteni Kalama na kuona iko haja ya kurejesha kundi kama zamani.``

Inspektah alisema marejeo mapya ya Gangwe ni kamilifu kwakuwa sasa wamepanga kufanya kazi upya pamoja -- kama zamani.

``Tumeshaanza kufanya `project` ya marejeo yetu na tayari tumesharekodi ngoma mpya kadhaa kwa ajili ya albam yetu ya kwanza tangu tulipotengana,`` alisema.

Miongoni mwa kazi mpya zinazoandaliwa na Gangwe Mobb mpya ni wimbo uitwao `Mwanzo Mwisho` unaomshirikisha muimbaji mkongwe wa dansi wa bendi ya Msondo Ngoma, Maalim Muhidini Gurumo.

``Tunaweka mambo sawa ili kutoka na mkongwe huyu. Tunajaribu kufanya muziki wa daraja tofauti na ushiriki wa Gurumo ni moja ya mikakati hiyo,`` alisema.

Katika marejeo hayo, Inspektah amesema wanatarajia kurejesha mtandao wao wa mavazi wa Gangwe Gear, tovuti yao na kila kitu kilichokuwa cha Gangwe. ``Tunataka kurejesha kila kitu cha kimaendeleo alichofungulia njia Sebastian Maganga (mtangazaji wa radio), alitupa mwelekeo mzuri sana,`` alisema rapa huyo.

Inspektah aliongeza kuwa kuungana upya na memba mwenzake wa Gangwe Mobb Luteni Kalama ni muendelezo wa urafiki wao wa miaka mingi ambao umefikia kuwa kama undugu.

``Hatujawahi kukorofishana na Luteni. Kilichotokea hadi kugawanyika kwa Gangwe ilikuwa ni katika kila mmoja kusaka maslahi zaidi.``

Baada ya Gangwe kugawanyika mwaka 2003, Inspektah alifanya kazi kivyake na tangu wakati huo ametoa albam nne za `Pamba Nyepesi` `Inabamba`, `Natega Mingo` na `Ndoa Haina Doa` iliyoingia sokoni miezi miwili iliyopita, wakati Luteni alijiunga na Wanaume TMK Family kabla ya kundi hilo kugawanyika wakati Juma Nature alipojitenga sambamba na nyota kadhaa -- Luteni Kalama akiwemo -- na kuanzisha kundi la Wanaume Halisi.

Inspektah aliongeza: ``Nami baadaye nikajiunga na Wanaume Halisi kwa lengo la kufuta hisia mbaya zilizojengeka kwa baadhi ya watu kuwa mimi nina bifu na Kalama au Nature au siwezi kufanya kazi na wenzangu.

Baada ya kutimiza hilo, hivi sasa nimerejea kwenye kufanya kazi zangu ndio maana nimejiondoa Wanaume Halisi, japo wakinihitaji ama nikiwahitaji tunaendelea kufanya kazi pamoja, sina ugomvi na yeyote.

``Na kuwemo kundini kulikuwa kunawanyima mashabiki wangu kunisikia kwa mapana.

Unajua mimi nina mashabiki wengi, sasa unapokua kwenye kundi kama vile mashabiki wanakusikia kwenye `bars` (mistari) mbili au tatu tu kwasababu wimbo mmoja unafanywa na watu kibao.

Hicho pia kimechangia kuamua kutoka ili nifanye albam yangu hii iliyopo sokoni ya `Ndoa Haina Doa`.

``Na Kalama kwa wakati wote hajafanya albam, hivyo ameona anahitaji kurejesha heshima yake, hivyo katika albam ya Gangwe atakuwa na `bonasi traki` zake ambazo atafanya peke yake.``

MIZIZI YA GANGWE
Historia ya kundi la Gangwe Mobb ilianzia mwaka 1994 wakati memba watatu wa kundi hilo Luteni Kalama, Inspektah na rapa Side Boy, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka saba tu, waliporekodi wimbo wao wa kwanza wa `Mauzauza` katika studio ya Mawingu chini ya mtayarishaji Bonny Luv.

Enzi ambazo Inspektah alisimulia kuwa prodyuza wao Bonny alilazimika kumwekea kistuli rapa Side Boy ili aweze kufikia `mic` wakati wa kurekodi studio.

``Mauza uza (ma) mauza uza ni kizazaa (ga) shaghala baghala,`` waliimba wasanii hao katika kiitikio cha wimbo huo uliowatambulisha katika gemu, kabla ya Side Boy kutojihusisha tena na kundi hilo.

Gangwe Mobb walitamba tena mwaka 1998 kwa kibao cha `(Mtu Bee) Chelea Pina` kabla ya kuja kufunika kwa mafanikio makubwa zaidi mwaka 2000 kupitia nyimbo zao za `Ngangari`, `Mtoto wa Geti Kali` na `Tunajirusha`walioimba na kundi la Neccessary Noize kutoka Kenya.

Na wakatesa hadi uzinduzi wa kishindo wa albam yao ya kwanza ya `Simulizi la Ufasaha` na wa albam yao ya pili ya `Nje Ndani` iliyotoka mwaka 2003 kabla ya Luteni kujitoa na kwenda kuasisi kundi la TMK Wanaume Family.

  • SOURCE: Lete Raha
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.