03 May 2009 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

KANONI :Beki wa Simba awazae ubingwa ligi kuu 2010
 
2009-05-03 18:45:53
By Ramadhan Mbwaduke

Pamoja na Simba kupata ushindi `mtamu` wa mabao 2-0 dhidi ya maafande wa Polisi Dodoma wiki iliyopita na hatimaye kutwaa tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika mwakani baada ya kumaliza wakiwa wa pili kwenye ligi kuu, bado kuna wachezaji ambao kiasi hawakuridhishwa.

Mmoja wa wale ambao furaha yao ina chembe ya sononeko, ni mlinzi Salum Kanoni wa \'Wekundu\' hao wa Mtaa wa Msimbazi.

Akizungumza na Lete RAHA jana Jumamosi, Kanoni anasema kuwa naye, kama walivyo wenzie kikosini, anayo furaha ya kuona chama lake likilinda heshima kwa `kujipoza` kwenye nafasi ya pili ya ligi kuu ya Bara.

Lakini, anasema kuwa furaha aliyo nayo yeye, kamwe haiambatani na kuridhishwa kwa asilimia mia moja na nafasi hiyo waliyotwaa kwa kufikisha pointi ambazo ni pungufu ya 10 za mabingwa Yanga waliomaliza wakiwa na pointi 50.

Akifafanua, Kanoni anasema kuwa mara zote, yeye na wenzake kikosini kwao, wanachowazia ni kutimiza lengo lao kuu la kuwa vinara wa kila shindano. Si kushika nafasi ya pili, nyuma ya timu hasimu kama watani zao wa jadi -- Yanga.

``Binafsi nimefurahi kuwa walau sasa tutaweza kuwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa,`` anasema Kanoni.

``Lakini japo nimefurahi, sijaridhika sana... naamini hata wachezaji wengine klabuni kwetu watakuwa kama mimi.

``Kwamba wamefurahi kidogo, ila hawajaridhika sana kwa kuona ubingwa ukitua kwa wengine (Yanga),`` anasema Kanoni.

``Simba ni timu kubwa. Simba ina vipaji vingi katika kila idara... kwa sababu hiyo na nyingine nyingi za kiufundi, naona wazi kwamba kinachopaswa kuturidhisha zaidi ni ubingwa pekee.

``Japo kushika nafasi ya pili ni kuteleza kuzuri, lakini hakuwezi kuturidhisha.

Lengo letu kuu ni kutwaa ubingwa na ninaamini kuwa kwa namna kila mmoja klabuni alivyopania, ni wazi kwamba msimu ujao utakuwa wetu,`` anasema Kanoni.

``Naamini hatutateleza zaidi... tena mambo mazuri yataonekana pia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.``

KANONI WA KANUNI
Mbali na kugusia `kanuni` za matarajio ya timu yake katika kuupoka ubingwa wa ligi kuu toka mikononi mwa Yanga msimu ujao, Kanoni ana kanuni zake nyingine uwanjani.

Siku zote, yeye si mtu wa papara. Hutulia katika kumsoma adui na kisha kumfuata akiwa tayari na uamuzi sahihi wa kufanya.

Atapiga chenga, atatoa pande la `akili` na pia atapanda kusaidia mashambulizi. Hachoki kirahisi.

``Huwa siku zote ninawazia namna ya kushirikiana na wenzagu katika kutekeleza maelekezo ya mwalimu na hatimaye tupate ushindi,`` anasema Kanoni ambaye ni beki mbili chaguo la kwanza Simba.

Kabla ya kutua Msimbazi, Kanoni ambaye ni `M-Kigoma` kama walivyo akina Mrisho Ngassa, Salum Swedi, Athumani Machupa, Juma Kaseja, Yahya Akilimali na nyota wengine, aliwahi kuzichezea Kigoma United, Villa Squad ya Magomeni Mapipa na Bandari Mtwara.
Humzimia zaidi kiungo Cesc Fabregas wa `chama` analolifagilia la Arsenal ya Uingereza.

  • SOURCE: Lete Raha
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.